2015-01-16

Balaa; WabungeDar hatarini kuteketea kwa moto

mng
SHABANI MATUTU NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
KAMATI ya Nishati na Madini, imeonyesha hofu juu ya Jiji la Dar es Salaam kuteketea kwa moto, kutokana na uwezekano wa kulipuka kwa mabomba ya kusafirishia mafuta kunakochangiwa na wizi wa mafuta unaohusisha utoboaji wa mabomba hayo.

Kutokana na hali hiyo, wabunge wametaka vyombo vya ulinzi, hususan Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wapewe jukumu la kulinda miundombinu ya kusafirishia mafuta, huku baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakijiandaa kuhamisha familia zao Dar es Salaam.

Hofu ya wabunge hao, ilitokana na taarifa iliyosomwa mbele yao na Meneja Mkuu wa Umoja wa Makampuni yanayoagiza Mafuta (PICL), Michael Mjinja, aliyeambatana na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Maji na Mafuta (Ewura) kwa ajili ya kutolea ufafanuzi punguzo la bei ya mafuta katika soko la dunia na namna punguzo hilo lisivyoweza kufanya kazi kwa wakati huo.

Katika sehemu ya taarifa yake, Mjinja alisema mafuta yanayopotea njiani baada ya kuibwa yanakuwa yameshalipiwa kodi hali inayowafanya waagizaji wabebe hasara hiyo.

“Mbali na kuibwa, mwenyekiti hatuombi litokee la kutokea, lakini kwa namna miundombinu ya kusafirishia mafuta ilivyo, ikitokea la kutokea hakutakuwa na Dar es Salaam, jiji lote litaangamia,” alisema Mjinja.

Kutokana na maelezo hayo, mjumbe wa kamati hiyo, Richard Ndasa, ambaye ni Mbunge wa Sumve (CCM), alisema Watanzania hawapaswi kufurahia kushuka kwa bei ya mafuta kama hakuna mkakati maalumu wa kulinda miundombinu yake.

Alisema ni jambo la hatari kama atatokea mwendawazimu na kufanikiwa kulipua miundombinu ya mafuta hali itakayofanya Ikulu ya Dar es Salaam iteketee.

“Tunao JKT na JWTZ, wakabidhiwe jukumu la kulinda miundombinu hii kwa kuwa tunao maadui, na hawa wengine hawahitaji hata kubeba bomu kwa ajili ya kujilipua zaidi ya kwenda na sigara yake na kusababisha madhara.

“Serikali yote ipo Dar es Salaam, kwa sasa tumshukuru Mungu nchi haina wendawazimu waliopitiliza, lakini tungeshaangamia na siyo hapa tu bali Tanzania nzima,” alisema Ndasa.

Alisema nchi ipo hatarini kulipuka kutokana na kupuuzwa kwa uwekezaji wa njia bora ya kusafirisha mafuta na kubaki kutegemea njia ya barabara.

Ndasa alisema ana taarifa ya mwekezaji aliyetaka kujenga mabomba ya kusafirisha mafuta kwa usalama kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze, lakini alikumbana na vikwazo mbalimbali.

Kauli ya Ndasa iliungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM), aliyesema wakati taarifa ya PICL ikisomwa, alikuwa anafikiria namna ya kuihamisha familia yake iwe mbali na Jiji la Dar es Salaam.

“Mwenyekiti kumbe tupo katika hatari kiasi hiki, hapa nilikuwa nafikiria kuwahamisha wanangu wawe mbali na Dar es Salaam kuepuka tishio hili,” alisema Mlata.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), alisema kutobolewa kwa mabomba na kisha maboya ya kujazia mafuta kutumiwa pasipo wahusika kubainika kwa wakati, kunadhihirisha namna bandari za Tanzania zisivyo salama.

Alisema kama kungekuwa na usalama katika Bandari ya Dar es Salaam, kusingetokea wizi wa aina yoyote unaoweza kuhatarisha mustakabali wa jiji zima kuteketea.

Alihoji sababu ya wauzaji wa mafuta kupandisha bei muda unaotangazwa kupanda mafuta na kuwa wazito kushusha bei wakati bei ya soko la dunia inapotangazwa kushushwa.
Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema), alisema waagizaji wa mafuta na Ewura, wanapaswa kueleza kwa kina kushindwa kushusha bei ya mafuta kwa wakati pale hali hiyo inaporuhusu.

Alisema wao kama wabunge wana taarifa hali hiyo inachangiwa na wafanyabiashara hususan wa vituo vya mafuta wanaodai walikuwa na akiba kubwa ya mafuta kabla ya bei kushuka.

Silinde alisema kuna mchezo mchafu unaofanywa na wafanyabiashara wa mafuta nchini kumzuia mwekezaji kutoka nchini Dubai asiingize mafuta ambayo yangechangia kwa kiasi kikubwa bei kushuka na kufikia Sh 1,500.

EWURA WAFAFANUA
Wakijibu madai hayo, maofisa wa Ewura wakiongozwa na Mhandisi Lorithi Long’itu, walisema kwa kawaida bei inayotangazwa katika mwezi husika, mafuta yanakuwa yameshaagizwa miezi miwili kabla.
Alitolea mfano mafuta yaliyonunuliwa Januari, mwaka huu baada ya kushuka kwa bei katika soko la dunia yataanza kuuzwa Machi.

“Kuna mambo matatu katika kushuka kwa bei ya mafuta kwa kuwa punguzo lolote linalofanywa katika soko la dunia litatafutiwa punguzo katika hilo tu na si katika kodi za ndani ambayo inachukua zaidi ya asilimia 30.

“Ili Watanzania waweze kununua mafuta ya petroli kwa Sh 1,200, bei katika soko la dunia itabidi iwe dola za Marekani 287 kwa metiki tani, kwa sasa tunanunua kiwango hiki kwa dola 750,” alisema Long’itu.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...