Mbunge wa Arusha Mjini, Gobless Lema (wa pili kushoto) akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai juzi baada ya kutoa ushahidi katika kesi ya utapeli inayomkabili Adam Abeid.
Ni siku moja baada ya Jaji mstaafu, Barnabas Samatta kutoa ushahidi katika kesi ya utapeli inayomkabili Adam Abeid Hai, Kilimanjaro.
Hai. Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amedai mshtakiwa aliyejifanya Jaji mstaafu, Barnabas Samatta, alimtisha kuwa angehakikisha anashindwa katika rufaa yake ya kupinga kuvuliwa ubunge.
Lema alidai kuwa baada ya kutotoa ushirikiano, mtu huyo alimtisha kuwa atahakikisha jimbo hilo linarudi CCM.
Lema alitoa maelezo hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa katika kesi ya kutaka kuwatapeli viongozi wa Chadema.
Mbunge huyo alitoa ushahidi siku moja baada ya Jaji huyo mstaafu kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo. Mbali ya Samatta shahidi mwingine, Profesa Abdallah Safari alitoa ushahidi.
Kesi hiyo inamkabili Adam Abeid, ambaye wakati kosa hilo linadaiwa kutendeka kwa kutumia simu, alikuwa ni mtahiniwa binafsi (private candidate) wa mtihani wa Taifa wa kidato cha sita.
Lema, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alitoa ushahidi wake juzi kwa kuongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Susan Kimaro.
Alisema mara tu baada ya kuvuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha 2012, alipokea taarifa kutoka kwa John Heche kuwa alikuwa akitafutwa na Wakili wa Chadema, Profesa Abdallah Safari.
“Nilimtafuta Profesa Safari akaniambia natafutwa na Jaji Samatta, akanipa namba yake nikampigia, lakini hakupokea akanitumia ujumbe yuko kwenye kikao nitume meseji,” alidai Lema.
Lema alidai baadaye mtu huyo aliyejitambulisha kama ‘Jaji Samatta’ alimtumia meseji akimpa pole kwa kuvuliwa ubunge na kuahidi angemsaidia na kila alipojaribu kumpigia alikuwa akitaka wawasiliane kwa meseji.
Aprili 12, 2012, Lema alidai kutumiwa meseji na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa iliyokuwa imetumwa kwake na mtu huyo aliyekuwa akijifanya Jaji Samatta ikisomeka:
“Mheshimiwa Slaa kesho nakwenda Dar kuonana na Chande ili tufanye mazungumzo ana kwa ana tujue nini kitaendelea, hivyo naomba unigharimie mafuta ya kwenda Dar.”
Lema alidai ujumbe huo ulimtia shaka kwamba wanayewasiliana naye siyo Jaji Samatta, bali ni tapeli na kumtumia meseji: “Wewe ni tapeli na tutakukamata.”
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment