2015-01-16

Huruma;Waethiopia 14 wadaiwa kutelekezwa chakani


Kibaha. Jeshi la Polisi limewakamata raia 14 wa Ethiopia kwa tuhuma za kukutwa katika moja ya vichaka vilivyopo eneo la Tamco, mjini hapa huku wakiwa hawana vibali vya kuingia nchini. 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Ulrich Matei alisema jana kuwa wahamiaji hao waliingia nchini wakitokea Kenya.


Alisema walisafiri kwa kutumia gari aina ya fuso hadi wilayani Bagamoyo walikotelekezwa kwenye moja ya mapori yaliyopo katika barabara ya Tamco.


Kamanda Matei alisema polisi kwa kushirikiana na idara ya uhamiaji waliwabaini wahamiaji hao baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.


Alisema raia hao walikuwa wakiona pikipiki zimebeba watu ambao siyo wenyeji wa eneo hilo, wakipitishwa kutoka chakani.


Kamanda Matei alisema walifuatilia na kuikamata pikipiki iliyokuwa ikitumika kuwasafirisha wahamiaji hao, baada ya dereva kukimbia na kuitelekeza. 
 



Alisema walifanya msako katika vichaka hivyo na kuwakuta wahamiaji hao.


Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Pwani, Grace Hokororo alisema waliwapokea watuhumiwa hao na tayari wamechukua maelezo yao.


Alisema katika maelezo yao, walidai kuwa wamekimbia njaa na vita nchini mwao na walikuwa wakijiandaa kusafiri kimya kimya hadi Afrika Kusini kutafuta kazi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...