Wafugaji 266 wa kijiji cha Mabwegere wilayani Kilosa mkoani Morogoro hawana makazi baada ya nyumba zao kuchomwa moto na wakulima.
Nyumba hizo zimechomwa moto baada ya kuzuka kwa mgogoro wa ardhi ambapo nyumba 38 zimeteketea kabisa na mazao ya chakula kuharibiwa huku baadhi ya wanawake na watoto wakilazimika kukimbilia kanisani kuomba hifadhi.
Wakizungumza kwa uchungu wanawake hao na watoto wamelalamikia baadhi yao kubakwa na kufanyiwa ukatili na wengine hadi sasa hawajulikani walipo ambapo wameeleza kupata hasara kubwa ya kuchomewa nyumba zao huku wakiiomba serikali kutizama upya mgogoro huo wa wakulima na wafugaji ili haki itendeke kwani mgogoro huo unawaumiza wanawake na watoto.
Mwandishi wetu ametembelea maeneo ya nyumba zilizochomwa moto na kukuta baadhi ya nyumba zikiendelea kuungua huku vyakula navyo vikiteketea kwa moto ambapo mwenyekiti wa kijiji na baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo wamesema chanzo cha mgogoro ni wakulima kuingia kwa nguvu katika mashamba ya kijiji cha wafugaji.
Baadhi ya vijana wa kimasai yaani morani wameonekana msituni wakiwa na silaha za jadi ambapo wamesema wanawasaka wakulima waliohusika na tukio hilo na kuendelea kulinda mipaka ya kijiji kuzuia wakulima wasiingie kwa nguvu.
Jeshi la polisi mkoa wa morogoro limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na askari wameonekana wakiwa na silaha wakiimarisha ulinzi katika kijiji cha Mabwegere
0 comments:
Post a Comment