2015-03-09

TFF isibadili kanuni kuwafurahisha wachache


 

Taratibu zinaelezwa kuwa ni kanuni au mpango unaotumika katika kufanya jambo fulani na desturi ni jambo la kawaida linalotendwa kila siku, mazoea, ada, kaida. Picha na Maktaba

Taratibu zinaelezwa kuwa ni kanuni au mpango unaotumika katika kufanya jambo fulani na desturi ni jambo la kawaida linalotendwa kila siku, mazoea, ada, kaida.

Kanuni ni neno la Kiswahili ambalo limezoeleka kutumika katika maisha ya kila siku. Kulingana na Kamusi ya Kiswahili Sanifu linaelezwa kuwa na maana ya desturi, kawaida, kaida, taratibu, nguzo, masharti au mila.

Taratibu zinaelezwa kuwa ni kanuni au mpango unaotumika katika kufanya jambo fulani na desturi ni jambo la kawaida linalotendwa kila siku, mazoea, ada, kaida.

Kwa ainisho hilo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya mchezo huo nchini ambalo limekuwa likidaiwa kubadili kanuni zinazosimamia uendeshaji wa Ligi Kuu ya Soka halina budi kukaa chini na kusoma vyema kanuni ambazo limejiwekea. 

Tunasema hayo kwa sababu TFF ikiwa msimamizi wa mchezo wa soka nchini haiwezi kukurupuka katika kuandaa utaratibu ambao utabadilishwa bila sababu za msingi.

Kwa zaidi ya wiki sasa, TFF haijasema wazi sababu za msingi za kufanya mabadiliko kwenye kanuni zake mbalimbali zikiwamo zinazohusu kadi zinazotolewa kwa wachezaji wa timu zinazoshiriki ligi hiyo.

Tunaamini, madai ya klabu ya Yanga ambayo baadaye yalithibitishwa na baadhi ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo kwamba TFF imebadili kanuni hizo kienyeji, bila kuzitaarifu wao kama klabu ambao ni wanachama wake, hili ni jambo linalotia shaka utendaji wa shirikisho hilo.

Pamoja na TFF kujitetea kwamba inayo kamati ya utendaji yenye jukumu la kubadili kanuni, lakini tunaamini wadau wake, zikiwamo klabu za soka lazima washirikishwe, waambiwe kila yanapofanyika mabadiliko yoyote kwenye kanuni.

Huo, hakuna shaka ndiyo msingi wa utawala bora ambao nchi yetu imejivunia kuwa nao, ambao tunaamini kuwa inafaa usiishie serikalini, bali kwenye idara, taasisi au hata vyama vya michezo.

Tunaamini, TFF inapokwenda Morogoro kwenye mkutano wa mwaka itajibu hoja zinazohusu baadhi ya kasoro ambazo zimejitokeza kwenye uendeshaji wake.
 Tunasema, pamoja na kuwa na ajenda zake ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya kujadiliwa wakati wa mkutano mkuu wa TFF kule Morogoro, tunaamini wajumbe watakuwa makini, watauliza au kuhoji sababu za msingi za mabadiliko ya kanuni hizo ambazo zimelalamikiwa na Yanga kwa madai kwamba zililenga kuwabeba wapinzani wao, Simba waliokuwa wakicheza nao jana. 

Tunadhani, wajumbe hao watakuwa wazalendo, watatambua kuwa wao ni wawakilishi wa vyama au familia ambazo zinaunda TFF na zinapojitokeza kasoro, lazima wazijadili, wasikae kimya wakati mambo yakiharibika.

Tathmini yetu inaonyesha kuwa hilo la kanuni siyo tatizo pekee kwa shirikisho letu, ambalo kwa mfano lilibadili kamati zake hivi majuzi zikiwamo za kisheria kwa maelezo kuwa kamati ya utendaji imeridhia jambo hilo lifanyike.

Tunaushauri uongozi wa TFF uwe makini wakati wa kufanya uamuzi wowote ambayo wakati mwingine badala ya kukuza mchezo wa soka katika nchi yetu, yanaudumaza.
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...