2015-01-27

Mambo Hayo;Wanaume Wadaiwa Kuwa Chanzo cha Mmomonyoko wa Maadili



TATIZO la kuporomoka kwa maadili ndani ya jamii ni kutokana na wanaume wengi kushindwa kutimiza wajibu wao ndani ya familia na jamii. 


Kauli hiyo ilitolewa juzi na Dk Chris Mauki, Mshauri wa Saikolojia na Mahusiano, ambaye pia ni Mhadhiri wa somo la Saikolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati wa semina ya kinababa iliyofanyika katika Ukumbi wa Makane uliopo Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Dk Mauki alisema mmomonyoko wa maadili unaotokea katika jamii yetu unasababishwa na wanaume kushindwa kutimiza wajibu wao kama wazazi na kuwaachia wanawake majukumu yote ambayo mengine yalipaswa yatimizwe na wanaume.

“Mmomonyoko wa maadili katika jamii ni matokeo ya wanaume kutowajibika kama wazazi na badala yake majukumu yao wameyatelekeza kwa wanawake.

“Wanawake wamekuwa na kazi nyingi kiasi kwamba wanazidiwa na hivyo kushindwa kudhibiti mwenendo wa maadili ya watoto wao ipasavyo,” alisema Dk Mauki.

Aliendelea kusema wanaume wengi wamekuwa na tabia ya kutelekeza familia zao na kutokomea pasipojulikana na kuwaachia wanawake mzigo mkubwa wa kutunza na kulea familia peke yao.

“Familia nyingi zinapokumbana na matatizo ambayo ni ya kawaida katika maisha ya binadamu kama maradhi, ulemavu au ugumu wa maisha, wanaume hushindwa kuwa wastahimilivu na hivyo huamua kutelekeza familia zao na kutokomea kusikojulikana,” alisema Dk Mauki.

Akirejea majukumu ya wanaume katika jamii, alisema wanaume ndio wasimamizi wa kila kitu katika familia, walezi, washauri, walinzi na watoaji wa mahitaji muhimu katika familia zao.

“Siku hizi wanawake wamekuwa ndio walezi wakubwa wa familia, kazi ambayo ilipaswa ifanywe na wanaume. Wanawake walipaswa kuwa walezi wa kisaikolojia na sio wahangaikaji wa kutafuta na kutunza familia, hii ilikuwa ni kazi ya wanaume,” alisema Dk Muki.

Akifungua semina hiyo, Mchungaji Debora Lusambi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kongowe, alisema kanisa liliamua kuandaa semina hiyo kwa wanaume kwani wanaume wameonekana kushindwa kutimiza wajibu wao ukilinganisha na wanawake.

“Kanisa limeona wanaume huingia kwenye ndoa bila ya kuwa na mafunzo yoyote ukilinganisha na wanawake ambao kabla ya ndoa hupata kufundwa maarufu kama ‘kitchen party’ na kumuaga binti yao ambayo hujulikana kama ‘send off’, vitu ambavyo huwasaidia kuwa walezi na wavumilivu katika ndoa zao.

“Hivyo tumeona ili kupunguza kuporomoka kwa maadili, ni lazima wanaume nao wapate mafunzo, watambue wajibu wao katika familia na jamii kwa ujumla,” alisema Mchungaji Lusambi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...