2015-01-19

Ni hatari sana: Tambwe nusu auawe






Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe (kushoto) akiwa amekabwa roba na mchezaji wa JKT Ruvu, George Osei (kulia).

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Amissi Tambwe, ameweka wazi kwamba mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting ambayo walimaliza kwa suluhu juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, haikuwa ya soka na yeye alinusurika kuuawa.


Beki wa Ruvu Shooting, George Osei (kulia) akimzongoza straika wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe.

Tambwe amesema ni mechi itakayobaki kwenye kichwa chake kwa mambo mawili, kwanza ni beki George Michael ‘beki mkatili’ ambaye alimpiga kiwiko kwenye jicho na mdomoni.


Pili ni maneno makali yaliyoupasua moyo wake baada ya kuitwa mkimbizi na kukumbushiwa vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini Burundi.


Beki wa Ruvu, Osei, akimdhibiti Tambwe.

Katika mahojiano na Championi Jumatatu, Tambwe amesema Michael alimkaba kwa nguvu zaidi ya mara moja na kumfanya ashindwe kupumua.

“Haukuwa mpira, hauwezi kuamini kama kweli wale walikuja uwanjani kucheza soka. Walinipiga kiwiko, wakanipiga ngumi na mwisho Michael alinikaba shingoni zaidi ya mara moja na kunifanya nishindwe kupumua.


Osei wa Ruvu akizikunja na Tambwe.

“Hii ni hatari, kuna mtu anaweza kuanguka akapoteza maisha siku moja. Wale wanajeshi hawaingii uwanjani kucheza soka, wanakwenda kucheza na mwili wa wachezaji wenzao.

“Ila nilishangazwa na mwamuzi kutoa kadi kwetu huku akionekana kuwahofia wanajeshi. Ukimwambia mwamuzi anachekacheka tu, sijui alikuwa anamaanisha nini.


Osei wa Ruvu akimzuia Tambwe asipelekea madhara langoni mwako.

“Nafikisha hata mashitaka kwa TFF, wawaangalie waamuzi na kuwasisitiza wafanye kazi yao kwa haki na kuwalinda wachezaji waliokwenda kucheza soka na si ugomvi,” alisema Tambwe na kuongeza.

“Kilichoniuma zaidi ni matusi na kuitwa mkimbizi, tena wakisema nimekimbia vita Burundi. Nimevumilia sana, ajabu wale ni askari lakini hawaonyeshi kuwa wanajua athari za vita.

“Vita Burundi, pia inaweza kutokea hapa. Hakuna anayetaka mabaya kama hayo, kumwambia mtu haujui kapoteza ndugu au vipi, si sahihi. Uliona Zidane alimpiga (Marco) Materazzi,” alisema kwa sauti ya taratibu.


“Sijalala, daktari wa timu aliniandikia dawa ya maji, nikaweka jichoni na pia ya kunywa. Bado jicho halioni vizuri.


Osei (kulia) akisukumana na Tambwe.

“Halafu si mimi tu, hata (Kpah) Sherman walimpiga kibao usoni, akashangaa kama soka Tanzania linachezwa hivi!

“Sijawahi kutamka hata siku moja, lakini leo ninatamka kuwa soka la hapa nchini hivi sasa ni vita na siyo burudani tena, haiwezekani mchezaji anacheza soka huku akirusha ngumi, viwiko na mateke uwanjani huku mwamuzi akiangalia tu bila ya kutoa maamuzi yoyote.

“Pia ninamshangaa huyu jezi namba 4 (George Osei), yeye kila ninapokutana naye lazima acheze kwa kunipania kwa kunicheza rafu za makusudi, kunirushia ngumi na viwiko, sasa angalia kama leo kanipasua mdomoni na jicho linaanza kuvimba, hapa ninapoongea na wewe nashindwa kuona mbele vizuri.”
 GPL.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...