2015-04-09

Zitto Kabwe Aanza Na Ngome Kuu ya CCM


Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anaanza ziara yake ya kwanza ya ujenzi wa chama hicho kipya mwishoni mwa wiki hii kwa kutembelea mikoa ambayo inachukuliwa kama ngome za Chama Cha Mapinduzi ( CCM ).

Zitto ambaye aliacha uanachama na ubunge wake wa CHADEMA mwishoni mwa mwezi uliopita, atafanya mkutano wake wa kwanza wa kisiasa mkoani Ruvuma.

Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa iliyobaki hapa nchini ambayo haijawahi kuwa na walau mbunge mmoja kutoka chama cha upinzani tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kwamba katika ziara hiyo, ACT-Wazalendo kinatarajiwa kufanya mikutano ya kisiasa kwenye mikoa 10 tofauti katika kipindi cha takribani wiki mbili. 
Kwa mujibu wa ofisa habari wa chama hicho,Abdallah Hamis, mikoa ambayo ACT kitaanza kujitangaza kwa mara ya kwanza ni Ruvuma,Njombe,Iringa,Morogoro,Dodoma,Singida,Tabora,
Shinyanga,Mara na Mwanza.

"Tutaanza mkoa wa Ruvuma mwishoni mwa wiki hii na kuelekea kwenye mikoa hiyo mingine kwa mujibu wa ratiba.Viongozi wa juu wa chama wamefanya uamuzi wa kuanza kazi na mikoa ambayo CCM imekuwa ikishinda.

"Ile kazi ya kufyeka pori ndo sasa inaanza rasmi.Chama kimeona itakuwa busara kuanza na maeneo mapya ambako kuna fursa nzuri zaidi ya kuleta mabadiliko.

"Baadaye tutakwenda kwenye mikoa mingine, lakini la msingi ni kuanza kazi katika maeneo magumu na kumalizia katika yale ambayo mbegu zimeshapandwa tayari,"alisema Hamis

Mikoa ya Ruvuma,Njombe,Morogoro,Dodoma na Tabora haina mbunge hata mmoja kutoka miongoni mwa vyama 22 vya upinzani vilivyopo hapa nchini,wakati mikoa ya Singida,Mara,Mwanza,Shinyanga na Iringa ina walau mbunge mmoja wa upinzani.

Akiwa Naibu katibu mkuu wa CHADEMA,Zitto alikuwa mmoja wa wahusika wakuu katika kile kilichoitwa "Oparesheni Sangara" iliyokuwa kampeni maalumu ya kukitangaza chama hicho katika mikoa ya kanda ya ziwa ambayo ndiyo inatajwa kuwa chachu ya kukua kwa ushawishi wa vyama vya upinzani kwenye mikoa hiyo.

Kwa mujibu wa Hamis,katika ziara hiyo,Zitto atafuatana na takribani viongozi wote wa juu wa chama hicho,akiwemo mwenyekiti Anna Mghwira, na katibu mkuu,Samson Mwigamba. 

Zitto na Mwigamba wanauzoefu wa kufanya mikutano ya hadhara katika sehemu mbalimbali hapa nchini tangu wakiwa CHADEMA,lakini kwa Mghwira hiyo itakuwa ni mara yake ya kwanza, akitarajiwa kuwa kivutio katika mikutano hiyo.

Mgwira ameingia katika historia ya Tanzania kama mwanamke wa kwanza kupewa wadhifa wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Siasa, baada ya kumshinda Estomil Mala katika uchaguzi wa ndani wa ACT uliofanyika jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa mwezi ulipita.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...