2015-02-21

DUUUUUUUUUUU NINGEKUWA MIMI CHENGE ,NISINGEDIRIKI KUJIITA NYOKA MWENYE MAKENGEZA


Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.

Kwako Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Niliwahi kuzungumza nawe kupitia ukurasa huu, nikakushauri kuhusu mambo fulani ambayo nashukuru kwamba licha ya kutopendezwa na lugha niliyoitumia kukufikishia ujumbe, angalau ulitekeleza baadhi ingawa siyo yote.

Ukajiuzulu wadhifa wako wa Uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti kutokana na sakata kubwa la Escrow ambalo nawe ulikuwa ukitajwa ndani yake ukidaiwa kuvuna shilingi bilioni 1.6.
Leo nataka kuzungumza nawe kuhusu kauli uliyoitoa hivi karibuni wakati ukiwahutubia wananchi wako katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mahaha, Kata ya Bunamala, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Mheshimiwa, nakuhakikishia kwamba ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, nisingethubutu kutoa kauli kama yako ya kujiita nyoka mwenye makengeza.

Mheshimiwa, unataka wananchi wako wasiamini kwamba wewe ni ‘mwizi’ kama ambavyo kelele zimekuwa zikipigwa kila kona bali unawataka waamini kwamba wewe ni mjanja wa kutafuta fedha, ukijifananisha na nyoka mwenye makengeza. Binafsi sijakuelewa kwamba kauli yako hiyo ilikuwa na lengo la kujisifia au vinginevyo.

Ukaenda mbali zaidi kwa kuwaambia wananchi wako kuwa kwenye ‘mchongo’ wa Escrow, ulienda pale kwa ajili ya kuwatafutia wananchi wako fedha kwa ‘ujanjaujanja’ na kwamba hustahili kuitwa mwizi kwa sababu hukuvunja duka la mtu, ukanukuliwa ukisema: “Tunatumia akili kutafuta pesa kwa ajili yenu.”

Unataka kusema kwamba wewe na wenzako mliotajwa kwenye Escrow mlikuwa mnatumia akili kujipatia fedha kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wenu? Ok, baada ya kutumia hizo akili zenu na kupata mabilioni, wananchi wako wamenufaika na nini?

Wizi ni wizi tu mheshimiwa, hata kama ukiingia duka la dawa kwenda kuiba dawa kwa ajili ya kumpelekea mwanao anayeumwa mahututi nyumbani, bado tafsiri ya wizi iko palepale. Nilitegemea katika kipindi hiki, ungeongozwa na busara zaidi kwa kutumia maneno ya hekima kusafisha taswira yako mbele ya watu wachache ambao bado wanakuamini lakini badala yake unatumia kauli za kujigamba kiasi hicho! Hii siyo sawa ‘Mzee wa Vijisenti’, kuwa makini na kauli zako!
Wasalaam.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...