2015-02-18

Gharama za simu mjadala mzito



Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Rene Meza, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu mwenendo wa kibiashara wa kampuni hiyo. Picha na Emmanuel Herman
Na Julius Mathias, Mwananchi.


Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeziagiza kampuni za simu kutoa maelezo kuhusu mabadiliko ya gharama za vifurushi vya muda wa maongezi, Vodacom Tanzania imeeleza kuwa mabadiliko hayo yanatokana na ongezeko la kodi na hivyo kulazimika “kubadili mazingira ya kibiashara ili kuepuka hasara”.

Kampuni nyingine kubwa ya mawasiliano, Tigo imeahidi kutoa ufafanuzi wa suala hilo kesho wakati Airtel imesema haijafanya mabadiliko yoyote kwenye gharama za vifurushi vyake.

Kumekuwapo na mijadala mingi katika mitandao ya kijamii kupinga bei mpya za vifurushi hivyo ambazo zimeelezwa kuwa ni megabati nane kwa vifurushi vyote vya saa 24, na megabati 60 kwa vifurushi vya wiki.

Bei hizo zinaelezwa kuwa zimeanza kutumika kwa wateja wanaotumia mitandao ya kampuni za Vodacom na Tigo, ambazo zinachuana vikali sokoni, huku baadhi ya wateja wa kampuni ambazo hazifanya mabadiliko ya gharama hizo wakiwashiwishi wenzao kuhama ili kutokuwa hewani kutokana na kukosa vifurushi.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema kuwa tayari mazungumzo kati ya mamlaka yake na kampuni hizo za mawasiliano yameshafanyika na kilichobaki ni wao kutoa maelezo ya hatua walizoichukua.

“Matumizi ya intaneti yameongezeka nchini na wananchi wengi wamekuwa hawajui namna ya kutofautisha vifurushi vya muda wa maongezi na vile vya intaneti. Lakini nimezungumza na kampuni zote na tumefikia mwafaka. Ndani ya wiki hii watatoa tamko lao pamoja na msimamo wa bei za vifurushi,” alisema Profesa Nkoma.

Machi, 2013, Profesa Nkoma alisema angehakikisha kampuni za simu zinawasilisha kwake makubaliano kuhusu punguzo la gharama za kupiga simu kwa mwingiliano wa mawasiliano, kutoka wateja wa kampuni moja kwenda nyingine.

Mabadiliko ya gharama na ukubwa wa vifurushi yalianza kujitokeza mwishoni mwa wiki iliyopita, hali iliyoibua mijadala mingi katika mitandao ya kijamii. Kilichojitokeza ni kwamba makampuni hayo yamepunguza ukubwa wa vifurushi vya intaneti na kutoathiri vile vya muda wa maongezi na ujumbe mfupi hali, iliyozusha hamaki kwa wateja wengi wanaotaka kujua sababu za mabadiliko hayo.


Baada ya mijadala hiyo kuongezeka, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba aliwaondoa wasiwasi wateja baada ya kuandika katika ukurasa wake wa facebook kuwa serikali imechukua hatua mara moja.


“Nimeongea na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma na nimemuagiza azungumze na kampuni za simu juu ya mabadiliko ya bei za bundles (vifurushi): ukubwa, ughafla na upamoja (mitandao yote). Nimewaagiza pia watoe majibu kwa umma haraka iwezekanavyo. Kampuni za simu hazipaswi kupanga au kuratibu kwa pamoja bei; tukigundua hilo limetokea ni ukiukwaji wa kanuni za ushindani wa soko,” inasema sehemu ya ujumbe huo.


Katika ujumbe wake, Makamba anafafanua kuwa Sheria ya udhibiti wa mawasiliano haiipi serikali nguvu ya kupanga bei, isipokuwa gharama za muingiliano “Inawezekana gharama za uendeshaji, ikiwamo umeme, zinapanda, lakini hakuna kodi mpya ya Serikali tangu baada ya bajeti. Huko nyuma 
ushindani ulishusha bei kwa sababu hakukuwa na bei elekezi. Bado niko nje ya nchi kwa safari ya kiserikali, lakini nimekuwa nalifuatilia suala hili kwa karibu. Pia nimeongea na Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Rene Meza, kuhusu suala hili leo asubuhi,” aliandika Makamba

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...