2015-02-06

Serikali yauchomoa Muswada wa Mahakama ya Kadhi bungeni




Msemaji Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame
 

“Wamefanya hivyo makusudi ili wananchi na Serikali wasitilie maanani maoni yaliyotolewa na taasisi 11, ambayo kama yatafanyiwa kazi na Serikali yatawezesha kupatikana kwa Mahakama ya Kadhi inayokidhi matakwa ya Sheria za Kiislamu na wajibu wake kama mamlaka ya kutoa na kutenda haki, ” Sheikh Rajab Katimba

Dodoma. Serikali imeuchomoa muswada wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi uliokuwa uwasilishwe bungeni ili yafanyike maridhiano kwanza.

Wakati Serikali ikichukua hatua hiyo, taasisi 11 za Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania zimeazimia kuwahamasisha wana jumuiya wake kususia Kura ya Maoni ya Katiba Mpya hadi watakapopata uhakika wa kuwa na Mahakama ya Kadhi yenye meno.

Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala iliyokutana jana mjini Dodoma ilielezwa kuwa Serikali imeomba muda wa kufanya maridhiano kabla ya kuwasilishwa muswada huo katika mkutano huu wa Bunge unaomalizika kesho. Ilielezwa kuwa muswada huo utawasilishwa katika mkutano ujao wa Bunge. 


Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kamati hiyo zinasema kuwa Bunge liliamua kuondoa muswada huo kujadiliwa pamoja na sheria mbalimbali na badala yake ujadiliwe peke yake.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali alisema katika kikao chao Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jasson Rweikiza aliwaeleza kuwa Serikali imeomba hivyo ili kufanya maridhiano na kuahidi kuwa itauwasilisha katika mkutano wa Bunge ujao.

Taasisi zapinga

Kauli ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu zipatazo 11 iliyotolewa Dar es Salaam jana na kusomwa na Naibu Katibu wa Jumuiya ya Shura ya Maimamu, Sheikh Rajabu Katimba ilisema itasusia mchakato wa Kura ya Maoni kwa madai kuwa kinachoendelea katika mchakato wa kupatikana kwa Mahakama hiyo ni hadaa za Serikali zinazofanyika miaka yote hasa kinapofika kipindi cha kupiga kura kwa lengo la kuungwa mkono na waumini hao.

Akizungumza kwa niaba ya jumuiya hizo zikiwamo, Baraza Kuu, Tampro, Basuta, Jasuta, IPC, Haiyat Ulamaa na Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Katimba alisema watawahamasisha Waislamu wanaounda Jumuiya hizo kutopiga kura ya maoni wala kushiriki kwa namna yoyote ile katika mchakato wa kupatikana Katiba Mpya kwa sababu haiitambui Mahakama hiyo.

Alisema mchakato wa kutoa maoni juu ya muswada unaohusu Mahakama ya Kadhi umepotoshwa kwa kuituhumu kuwa italeta vurugu ikiwamo kuhukumu kwa kukata watu mikono, kuhukumu wasiokuwa Waislamu na kuwabagua wasiokuwa Waislamu na kwamba ni upotoshaji wa makusudi ukiwa na lengo la hadaa. 


“Wamefanya hivyo makusudi ili wananchi na Serikali wasitilie maanani maoni yaliyotolewa na taasisi 11, ambayo kama yatafanyiwa kazi na Serikali yatawezesha kupatikana kwa Mahakama ya Kadhi inayokidhi matakwa ya Sheria za Kiislamu na wajibu wake kama mamlaka ya kutoa na kutenda haki,” alisema Sheikh Katimba.

Hata hivyo, Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa Shaaban Simba alisema Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba Sheria na Utawala ilipata maoni ya taasisi zote za Kiislamu na kila moja ilitoa maoni ya nini kifanyike ili kuboresha muswada wa Mahakama ya Kadhi.

Alisema Bakwata iliungana na Serikali na kukubaliana nini kitoke, kibaki, kiboreshwe na kusema taasisi hizo nazo zilipaswa kutumia wakati huo kukubali, kukataa, kutoa mapendekezo, kujadili.
Mwananchi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...