Viongozi wa madhehebu ya dini jijini Mwanza, wakiwamo Maaskofu na Mashehe jana walijikuta wakibubujikwa na machozi baada ya kumtembelea Ester John, ambaye amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Ester amelazwa baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiofahamika, ambao walimteka mwanawe mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Yohana Bahati na kutokomea naye kusikojulikana.
Viongozi hao wakiwemo maaskofu 10 na mashehe 10 walimtembelea Ester hospitalini hapo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kongamano kubwa la amani linalotarajiwa kufanyika Februari 28 mwaka huu kuiombea nchi amani na kulaani mauaji ya albino.
Mashehe na maaskofu hao walimuombea dua na sala Ester aweze kupona haraka na walilaani kitendo cha kinyama, alichofanyiwa na wauaji hao.
Waliiomba Serikali ichukue hatua za haraka kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.
Akizungumza hospitalini hapo huku akitokwa na machozi katika Wadi Namba 9 alikolazwa Ester, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa ya Viongozi wa Dini, Shehe Hassan Kabeke alisema wanaungana kwa pamoja kulaani matukio mawili ya kinyama ya kuuawa kwa mtoto Yohana na kujeruhiwa vibaya mama yake mzazi.
“Maneno ya kusema yananiishia baada ya kumuona Ester, mimi nadhani hakuna sababu ya kuremba maneno dhidi ya ukatili huu wa kinyama, nasikia maumivu makali sana ndani ya moyo wangu kama kiongozi wa kiroho, tunaitaka serikali katika hili isiondoe adhafu ya kifo kwa kisingizio cha haki za binadamu”, alisema.
Aliongeza “Tunapozungumzia haki za binadamu, maana yake ni usawa, ukweli na haki kwa watu wote nchini, haiwezekani watu wengine waue watu halafu tunasingizia haki za binadamu, na wao wahukumiwe adhabu ya kifo, katika hili msimamo wetu kama viongozi wa dini tunaomba adhabu ya kifo isiondolewe”.
Pia, aliwataka majaji wanaosikiliza kesi za watu wenye ulemavu wa ngozi, kuzisikiliza kwa wakati ili kuondoa ucheleweshaji wa kesi hizo ili hukumu zitolewe kwa wakati.
“Nichukue fursa hii kwa niaba ya wenzangu kuwaomba waheshimiwa majaji waharakishe kusikiliza mashauri yaliyoko mahakamani yanayohusisha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino)”, alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mwenza wa Kamati hiyo ya Amani, Askofu Zenobius Isaya alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu kulichukulia suala la mauaji ya albino kwa uzito wa kipekee kwa vile linagharimu maisha ya watu wasio na hatia katika jamii.
“Tunamuomba IGP Mangu alichukulie suala hili kwa uzito mkubwa, afanye uchunguzi wa kina ili aweze kukomesha mauaji haya ambayo yameipaka matope nchi yetu mbele ya Jumuiya ya Kimataifa”, alisema.
Akitoa salaam kwa Ester ambaye aliweza kukaa kitandani kwa muda, Isaya alisema shida iliyomkuta ni shida ya Watanzania wote wenye kupenda amani na kuchukia maovu.
“Shida iliyokukuta na taabu yako ni taabu yetu sisi sote wapenda amani ; na sisi wapenda amani kwa wingi wetu, kama unavyotuona, tunalaani tukio hili la kinyama, jambo hili ni la kinyama lakini tunakutia moyo uweze kupona haraka na Mungu akupe moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu,” alisema.
Aliushukuru uongozi wa Hospitali ya Bugando kwa kufanya kazi kwa uvumilivu na kutanguliza upendo katika kumhudumia Ester tangu alipolazwa hospitalini hapo Februari 17 mwaka huu.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru sana madaktari na wauguzi wetu kwa kuwa bega kwa bega na Ester kwa kumhudumia bila ya kuchoka, hii inaonyesha kuwa na mshikamano na Mungu awabariki”, alisema.
Awali, akiupokea ujumbe huo, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Hospitali ya Bugando, Leah Kagina aliwashukuru viongozi hao wa dini kwa kuamua kutenga sehemu ya muda wao kwa kwenda kumjulia hali.
Alisema hiyo ni mara ya kwanza kwa hospitali hiyo kupokea ujumbe huo mkubwa kwenda kumjulia hali Ester.
“ Tunawashukuru sana kwa ujio wenu, ni kwa mara ya kwanza kwa hospitali kupokea ujumbe huu mzito wa viongozi wa kiroho kwa ajili ya kuja kumjulia hali Ester, hii inadhihirisha ni jinsi gani mlivyo na upendo kwa watu wote, rai yangu kwenu niwaombe mtumie ibada zenu katika kutoa elimu kwa jamii dhidi ya mauaji haya”, alisema.
Alisema kuwa viongozi wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii juu ya imani potofu, ambazo zimekuwa zikienezwa dhidi ya mauaji hayo na kuitaka serikali kuwachukulia hatua stahiki wauaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi.
Akizungumzia hali ya mgonjwa, Muuguzi wa Zamu katika wadi Namba 9, alikolazwa Esta, Adolphina Kishumba alisema hali ya Ester kwa sasa inaendelea vizuri na anajitahidi kula chakula.
“Kwa hivi sasa hali ya Ester inaendelea vizuri, ni tofauti na alivyokuwa mwanzo na sasa hivi anakula na anaanza kutembea kwenda chooni”, alisema.
Mama mzazi wa Ester ambaye anamuuguza hospitalini hapo, Tabu Mang’enyi aliwashukuru Watanzania kwa misaada yao ya hali na mali wakati wote, ambao amekuwa na mwanawe hospitalini hapo.
“Nawashukuru Watanzania wote kwa kumuombea mwanangu na kuendelea kumjulia hali. Kutokana na maombi yenu hali ya mwanangu inaendelea vizuri”, alisema.
0 comments:
Post a Comment