Mlipuko wa kipindupindu ulioukumba mkoa wa Kigoma, umesababisha vifo vya watu watano, huku wengine zaidi ya 170 wakilazwa hospitalini.
Hayo yalithibitishwa mjini hapa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Leonard Subi (pichani) akisema Manispaa ya Kigoma/Ujiji imeathirika kwa kiasi kikubwa na ugonjwa huo, na kwamba tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa kukabiliana na hali hiyo.
Alisema tangu Januari mwaka huu, ugonjwa huo ulioanza kuripotiwa kwenye wilaya ya Kasulu na Manispaa ya Kigoma/Ujiji, watu 175 walikuwa wamekumbwa na ugonjwa huo katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji huku Kasulu ikiwa na wagonjwa wanane.
Alisema kwa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, eneo lililoathiriwa ni Kata ya Kibirizi ambako sehemu kubwa ya wagonjwa waliougua na kufariki walitoka huko na kwamba tayari kambi ya wagonjwa wa kipindupindu imefunguliwa kwenye kituo cha afya cha Gungu, Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Akizungumzia hali hiyo, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, John Maginga alisema hatua za kudhibiti ugonjwa huo zimeshachukuliwa, ikiwemo kuvifunga baadhi ya visima ambavyo vimegunduliwa kuwa na vimelea vya ugonjwa huo.
Hata hivyo, alisema kufungwa kwa visima vitatu vya Senzia, Kibore na Msulula B ambavyo viligundulika kuwa na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu hakukubaliwa na wananchi wa eneo hilo la Kibirizi, kwani wananchi waliendelea kuvitumia visima hivyo kwa siri usiku, jambo ambalo limelilazimu mamlaka kuweka ulinzi ambao unavilinda visima hivyo kwa masaa 24.
Mganga huyo wa Manispaa alitaja hatua nyingine ambazo zimechukuliwa kuwa ni pamoja na kufunga shughuli zote za uuzaji vyakula magengeni (mama ntilie), kutoa elimu kwa njia ya magari, kusambaza vipeperushi kwenye maeneo ya mkusanyiko, ikiwemo kwenye nyumba za ibada kwenye masoko na vituo vya magari.
Hofu zaidi iko katika vyombo vya usafiri, kwani Kigoma ni moja ya mikoa inayoingiliana na mikoa mingi nchini, hasa kutokana na usafiri wa treni unaoanzia Dar es Salaam na kupitia mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora ambako baadhi ya mabehewa hugawanya na kwenda Mwanza na Shinyanga, huku mengine yakienda Mpanda mkoani Katavi.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Kigoma - Ujiji wamelalamikia kukithiri kwa uchafu katika manispaa hiyo kunakotokana na kuzagaa kwa uchafu kufuatia ofisi ya afya ya Manispaa hiyo kushindwa kuzoa taka zinazokusanywa kwenye vizimba na mitaani.
0 comments:
Post a Comment