2015-02-20

MBASHA PUNGUZA MUNKARI!...........soma hapa kilichojiri




EMMANUEL Mbasha ana jina kubwa katika muziki wa Injili hapa nchini. Lakini hata hivyo, ukubwa wa jina lake hautokani na uwezo wake wa kuifanya kazi hiyo, bali kitendo chake cha kufunga ndoa na mmoja kati ya waimbaji bora zaidi wa kike, Flora Mbasha.

Simfahamu sana kikazi Emmanuel, lakini nimewahi kusikiliza nyimbo zake kadhaa na kugundua kuwa anacho kipaji kinachohitaji kuendelezwa. Anafanya kazi nzuri ya utumishi wa Mungu kwa kuwaelekeza watu njia ya kupita ili kuepuka matendo mabaya, kama waimba Injili kote duniani wanavyowafundisha mafuasi wao.

Katika miezi ya karibuni, uhusiano wake na mkewe uliingia dosari kiasi cha kujikuta mambo yao ya chumbani yakiibuka hadi sebuleni kabla ya kuingia mtaani na kuwa habari kubwa ya mjini. Ndoa yao ipo katika msukusuko mkubwa unaohatarisha ustawi wake.

Katika nafasi yangu ya uandishi, nimesikia kauli zao mara kadhaa, kila mmoja akiitoa kwa namna ya kumshangaa na hata kumshambulia mwenzake. Kwa watu walio katika maisha ya ndoa kama mimi, habari zao zinahuzunisha sana kwa sababu zinajaribu kukuweka katika nafasi ambayo haungependa ikukute siku moja.

Kuzungumza mambo ya ndani ya mke au mume wako siyo jambo linalopendeza hata kidogo, kwa sababu ni watu wanaofahamiana kwa mambo yao mengi ndani ya nyumba yao. Niliwahi kuzungumza suala hili wakati ule Gardner alipotofautiana na mkewe Jide na kila mmoja kuanza kumzungumzia mwenzake kwa maneno mabaya katika vyombo vya habari.

Jambo hili limejitokeza tena kwa wanandoa hawa, ambao mzozo kati yao umewaweka mbali kimaisha, kila mmoja akiishi kivyake. Nimejikuta nikiumizwa zaidi na Emmanuel katika mzozo huu, kwa sababu yeye ni kijana wa kiume, ambaye mara nyingi, tunaamini ni wavumilivu na wenye subira zaidi kuliko akina dada.

Amezungumza maneno mengi kuhusu mkewe, hadi kumtupia baadhi ya tuhuma ambazo kimaadili, alipaswa kubaki nazo kama siri yake moyoni. Moja kati ya mambo hayo ni tuhuma kuhusu ujauzito uliosababisha kujifungua mtoto hivi karibuni.

Wakati ninamsifu Flora kwa kuulea ujauzito wa mtu ambaye anachafuana naye magazetini na mitandaoni, nimeshangazwa kidogo na Emmanuel kwa kumkana mtoto aliyezaliwa, akitaka jamii ielewe kuwa mkewe amechepuka.

Lakini maneno ya baba mdogo wa Flora aliyejitambulisha kama Kisekwa, aliwaambia waandishi wa Global Publishers kwamba maneno ya mkwe wake ni ya kushangaza sana kwani kila ndugu wa pande zote, wanafahamu kwamba wakati mzozo kati yao ukianza, mwanamke alikuwa ni mjamzito na wote wawili walifahamu kuhusu jambo hilo.

Kama ukweli ni huu, kwa nini Emmanuel anajaribu kukifanya kitu cha namna hii, hasa kwa mtu ambaye anafahamika kama Mtumishi wa Mungu? Anataka dunia ifahamu kwamba Flora alizini nje ya ndoa yake na asivyo na busara, akamudu hata kuzaa nje katika kipindi kifupi tu cha mzozo wao? 

Lakini kwamba ujauzito siyo wake, yaweza kuwa kweli pia kwani hakuna lisilowezekana chini ya jua. Kinachonitatiza ni ukosefu wa busara za kawaida tu za kibinadamu katika kupambanua mambo, hasa ya kifamilia kama haya.

Leo wapo katika mzozo, vipi kesho wakifikia mahali na kumaliza tofauti zao? Mbasha hatajisikia vibaya tukimwambia analea mtoto asiye wake?Mtoto wa kiume siku zote anatakiwa kuwa jasiri na mvumilivu, ndiyo maana wazee wenye busara zao husema mwanaume ana koromeo, linalomzuia kuongea baadhi ya mambo.
 Muache mtoto wa kike apige kelele kwa sababu ndiyo sifa yao ‘kuchonga’, wanaume wanatafuta hela. Andiko hili liwahusu pia wanandoa wengine wote wanaokimbilia kuzungumza habari za wenza wao nje kutokana na mzozo wao. Unaweza kudhani unamkomesha mwenzako, lakini ukweli ni kwamba unajivua nguo mwenyewe!
GPL

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...