2015-02-19

Mtoto albino aliyenyang'anywa mikononi mwa mamaye akutwa amekatwa miguu, mikono yote. Kiwiliwili chake chatelekezwa msituni



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo.


Siku tatu baada ya mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Yohana Bahati (1), kutekwa na watu wasiofahamika, hatimaye mwili wake umepatikana ukiwa umekatwa miguu, mikono yote na kiwiliwili chake kufukiwa shambani katika Kitongoji cha Mapinduzi, Kijiji cha Rumasa ndani ya hifadhi ya msitu wa Biharamulo Wilaya ya Chato, mkoani Geita.

Mtoto huyo alinyakuliwa Jumapili iliyopita nyumbani kwao saa 2:15 usiku akiwa amebebwa na mama yake mzazi, Esther Jonathan (30), baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa mapanga usoni, mwili wake ulipatikana baada ya msako uliofanywa na wananchi.

Akizungumza na NIPASHE jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alisema mwili huo ulipatikana juzi saa 12:30 jioni katika shamba la mahindi lisilo rasmi kutokana na kulimwa ndani ya hifadhi ya msitu wa Biharamulo, wilayani Chato.
 Mwili huo ulipatikana kutokana na jitihada za wananchi walioshirikiana na makachero wa Jeshi la Polisi baada ya mwananchi mmoja (jina wanalo polisi) kuonekana akikatisha katika msitu huo, huku upande wa shati lake ukionekana ukiwa na damu.

Kamanda Konyo alisema baada ya raia huyo kuona viashiria hivyo, alilazimika kutoa taarifa kwa wananchi wenzake, ambao walifuatilia mwelekeo wa nguo hiyo na kufanikiwa kuona shimo limefunikwa na udongo mbichi kisha walipofanikiwa kufukua wakauona mwili huo.

“Baada ya wananchi hao kufukua shimo hilo, walifanikiwa kukuta mwili wa mtoto Yohana ukiwa umekatwa mikono na miguu yote...
baadaye mwili huo ulichukuliwa na askari hadi katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Kamanda Konyo.

Hata hivyo, baada ya kuupata mwili huo, wananchi hao walipandwa na jazba na kumtuhumu mwananchi huyo kuhusika na mauaji hayo na kuanza kumshambulia kabla ya polisi kuingilia kati na kumuokoa kutoka mazingira hayo.

“Hivi sasa tunamshikilia mtu huyo pamoja na baba wa marehemu, Bahati Misalaba, kwa ajili ya upelelezi zaidi, kwa sasa hatuwezi kumtaja jina ili kutovuruga uchunguzi wetu,” alisema Kamanda Konyo.

Alisema lengo la jeshi hilo lilikuwa kuhakikisha mtoto huyo anapatikana akiwa hai, lakini jitihada zao ziligonga mwamba baada ya kubaini tayari watekaji wamemuua.

Aliwataka wananchi kujiepusha na imani za kishirikina kwa kuwa zinasababisha maafa makubwa na fedheha ndani na nje ya nchi.

“Naomba wananchi watambue hakuna utajiri wala cheo kinachopatikana kwa kumuua albino. Hizo ni imani za kijinga kabisa. Bali mafanikio yanapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa,” alisema Kamanda Konyo.

Wakati tukio hilo linatokea, baba wa familia, Bahati Misalaba (39) alikuwa nje ya nyumba yao anaota moto na hakujeruhiwa, huku watoto wake wengine wawili albino; Shida (11) na Tabu (3) wakicheza nyumba za jirani na hivi sasa wamehifadhiwa sehemu nyingine.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa, wameingiwa na hofu na kuhusisha tukio hilo na wanasiasa na wafanyabiashara, ambao hudanganywa na waganga wa kienyeji kuwa wakitumia viungo vya albino watanyookewa na mambo yao.

Kwa mujibu wa idadi ya waganga wa jadi kwa baadhi za wilaya za Mkoa wa Geita, ni kubwa sana kwa mujibu wa Afisa Utamaduni Wilaya ya Geita, Mufungo Paulo, akidai zaidi ya waganga 900 wanatambuliwa wilayani mwake, wilayani Chato (265) kwa mujibu wa John Katunzi na Bukombe wapo zaidi ya 600.

Wakati mwili wa mtoto huyo unapatikana, hali ya mama yake mzazi, Esther, inazidi kuwa mbaya kutokana na hivi sasa kupumua kwa taabu na mwili kuvimba.

Akizungumza na NIPASHE jana, Dk. Derick David, ambaye ni mkuu wa kitengo cha dharura katika hospitali ya Rufaa ya Bugando, jijini Mwanza, alisema hali ya mama huyo inazidi kuwa mbaya kutokana na majeraha aliyoyapata wakati watu wasiojulikana walipomcharanga mapanga na kumpora mtoto wake aliyekuwa amembeba.

Dk. David alisema hivi sasa Esther anatumia mipira kwa ajili ya kumsaidia kupumua kutokana na hali yake kuwa mbaya.

Kutekwa kwa mtoto Yohana, kunafuatia siku ya 54 tangu kutekwa mtoto mwingine albino, Pendo Emmanuel (4) wa Kijiji cha Ndami, wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, Desemba 27, mwaka jana.

Mpaka sasa pamoja na juhudi za polisi na wananchi, mtoto Pendo hajaweza kupatikana.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...