Kesi za watuhumiwa wa rushwa zisipite kwa DPP.
Dodoma. Wabunge jana walikoleza jitihada za kutaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ipewe mamlaka ya kufikisha watuhumiwa mahakamani, wakisema ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) pamoja na viongozi wa juu wanazima mashauri mengi.
Takukuru ni chombo kilichoanzishwa chini ya Sheria Namba 11 ya Takukuru ya mwaka 2007, kikiwa na uwezo wa kuchunguza na kufikisha mahakamani watuhumiwa wa rushwa ndogo, lakini hakina mamlaka ya kuwafikisha mahakamani mawaziri na vigogo wengine kwa kuwa kinatakiwa kuwachunguza na kufikisha majalada yao kwa DPP ambaye ana uamuzi wa kuwafungulia mashtaka.
Jambo hilo limekuwa likichukuliwa kuwa ni udhaifu wa sheria hiyo na wabunge wamekuwa wakitaka Takukuru iongezewe meno ili kiweze kufungua mashtaka dhidi ya watuhumiwa vigogo.
Akiwasilisha bungeni taarifa ya mwaka ya shughuli za kamati yake, mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Jasson Rweikiza alisema Takukuru kwa sasa ina uwezo wa kutosha kujisimamia kwa kuwa na rasilimali watu na nyenzo za kazi, tofauti na ilivyokuwa awali ilipokuwa na upungufu wa rasilimaliwatu na kulazimika shughuli za kufungua na kuendesha mashtaka mahakamani kusimamiwa na DPP.
“Kitendo cha kuomba kibali kwa DPP kinaathiri utendaji wa Takukuru kwani inapeleleza tuhuma nyingi ambazo hatimaye hukosa kibali cha DPP kwa kigezo cha kukosa ushahidi,” alisema Rweikiza.
Alisema jambo hilo limekuwa likidhoofisha juhudi za Takukuru katika mapambano ya rushwa, kwani vibali huchelewa kutolewa na wakati mwingine havitolewi kabisa.
“Gharama nyingi za serikali zimekuwa zikitumika katika kufanya uchunguzi wa tuhuma za rushwa, lakini majalada yanapowasilishwa kwa DPP, mengi hayatolewi vibali na kuachwa kwa kigezo cha kutokuwa na ushahidi wa kutosha, jambo linaloisababishia hasara Serikali,” alisema Rweikiza.
Alisema katika kipindi cha kuanzia Julai 2014 hadi Januari 2015, Takukuru imechunguza majalada 3,014 ya rushwa na kati ya hayo Takukuru imefungua kesi 108 mahakamani.
“Idadi hii kubwa ya majalada yanayochunguzwa ni kielelezo cha nchi yetu kuchukia rushwa na kuchukua hatua stahiki kwa wale wanaothibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa,” alisema.
Akichangia hoja ya kamati hiyo Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya alisema sheria ya Takukuru ibadilishwe kwa taasisi hiyo iweze kuchunguza na kushitaki ili wala rushwa wapelekwe mahakamani.
Alisema walarushwa wadogowadogo ndiyo wamekuwa wakifikishwa mahakamani lakini wale wakubwa hawafikishwi nkutokana na Takukuru kutokupewa meno.
Sakaya alisema nchi inanuka rushwa kwa kuwa hata mahakamani ambako ndiko kunatolewa haki rushwa hivi sasa inapita kwa kuwa usipokuwa na fedha unafungwa hivihivi.
Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment