WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, atatoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali (GN) juu ya tozo mpya za hoteli za kitalii, baada ya kufanya upya ukokotoaji kwa kutumia kanuni namba 50 ya mwaka 2002.
Kauli ya Waziri Nyalandu, imekuja siku moja baada ya maazimio ya Bunge kumtaka kutoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali (GN) kuhusu kuanza kutoza tozo mpya ya hoteli za kitalii zilizopo kwenye hifadhi za taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri Nyalandu, alisema kanuni namba 50 ya sheria ya 2002, inataka malipo hayo yatozwe kwa asilimia, badala ya kukadiria kama baadhi ya watu wanavyotaka afanye.
Alisema si kweli kama alikataa kusaini na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 80, bali alitaka ukokotoaji wa tozo hizo ufanywe upya, baada ya kubaini udanganyifu uliofanywa na wataalamu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), ambapo baadhi ya hoteli hazikuwa zimejumuishwa katika ulipaji wa tozo mpya.
Nyalandu alisema kamwe hapingani na Bunge linalomtaka atoe tangazo hilo ifikapo Februari 28.
“Nia yangu ni kutaka hoteli zote zilizopo katika hifadhi za taifa zijumuishwe katika utozwaji wa tozo hizi kulingana na hadhi ya kila moja,” alisema Waziri Nyalandu.
Alisema kama angekubali kusaini tangazo hilo, tozo mpya zingekusanywa kwa hoteli 27, badala ya 56 zilizopo katika hifadhi za kitalii, jambo ambalo lingeikosesha Serikali mapato makubwa.
Juzi, Bunge lilitoa azimio la kumtaka Waziri Nyalandu kutekeleza amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ya Septemba, mwaka jana, iliyomtaka hadi kufikia Januari 28, mwaka huu awe ametoa tangazo katika Gazeti la Serikali ili kuruhusu tozo mpya kuanza kulipwa.
“Napenda Watanzania wanielewe, si kwamba niligoma kusaini tozo mpya, nilitaka ukokotoaji ufuate ‘formula’ (kanuni) iliyo sawa, siwezi kuruhusu tozo hizi zilizokokotolewa “kishkaji’ kwa sababu hoteli zinazidiana hadhi katika hifadhi zetu, hivyo haiwezekani zikatozwa kwa bei zilizo sawa, nitakuwa nimeumiza Watanzania,” alisema.
Wakichangia taarifa ya utekelezaji wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira bungeni juzi, baadhi ya wabunge walimnyoshea kidole Nyalandu, wakimtaka ajiuzulu kutokana na kushindwa kutekeleza amri ya mahakama iliyomtaka kutoa tangazo la Serikali linalotaka hoteli zote za kitalii kutozwa tozo mpya kwa mfumo wa ‘fixed rate’ badala ya mfumo wa zamani wa ‘concession rate’.
0 comments:
Post a Comment