SIRI ni moja ni kuwa kama Real Madrid inahitaji kutwaa ubingwa wa La Liga msimu huu basi inatakiwa kuhakikisha haipotezi mchezo wa keshokutwa Jumapili dhidi ya Barcelona kwenye Uwanja wa Camp Nou.
Real Madrid imetwaa ubingwa katika misimu minne ya 2011-12, 2007-08, 2006-07 na 2002-03 ambayo haikufungwa uwanjani hapo.
Wakati takwimu zikieleza hivyo kikosi cha Madrid kinachoongozwa na Kocha Carlo Ancelotti kinaonekana kutotulia huku vita ya wachezaji mastaa ikidaiwa kuigawa timu hiyo, wakati wenzao, Barcelona wanaonekana kutulia huku makali ya Lionel Messi yakiongezeka.
Madrid imekuwa na mwendo wa kusuasua tangu kuanza kwa mwaka huu na inadaiwa kuwa mastaa wake, Cristiano Ronaldo na Gareth Bale hawana uhusiano mzuri.
Upande wa Messi ameongeza kasi ya kufunga mabao ambapo miezi miwili iliyopita alikuwa amezidiwa mabao 12 ya kufunga na Ronaldo, lakini mpaka sasa Messi anaongoza katika ufungaji akiwa na mabao 32 huku Ronaldo akiwa na 30.
Akizungumzia mechi hiyo, Luis Suárez wa Barcelona anasema yupo tayari kwa ajili ya mchezo huo kwa kuwa anajua historia na umuhimu wake ni mkubwa.
“Nakumbuka ule ushindi wa mabao 5-0 (wa Barcelona), nilikuwepo uwanjani siku hiyo, niliona mambo mengi jinsi watu walivyoshangilia lilikuwa jambo zuri na la kipekee,” alisema Suarez.
Aidha, kurejea uwanjani kwa kiungo, Luka Modric kunadaiwa kuamsha morali ya Bale ambaye hakuwa kwenye kiwango kizuri kwa muda. Modric alikuwa nje kwa muda mrefu, katika mechi iliyopita alicheza na Bale akafunga mabao mawili, wawili hao walicheza pamoja Spurs kabla ya kutua Madrid.
0 comments:
Post a Comment