2015-03-24

Ukawa kujadili mvutano wa majimbo Ijumaa


  Viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)

Taarifa kutoka ndani ya wanachama wanaounda umoja huo, zinaeleza kwamba, viongozi watakaokutana ni wenyeviti wa vyama, makamu wenyeviti, makatibu na wajumbe wa sekretarieti kutoka ndani ya vyama hivyo.

Viongozi wa ngazi za juu wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watakutana Ijumaa wiki hii kutafuta mwafaka katika mvutano uliopo katika majimbo 19 ya uchaguzi, yakiwamo manne ya Dar es Salaam, Mwananchi limedokezwa.

Taarifa kutoka ndani ya wanachama wanaounda umoja huo, zinaeleza kwamba, viongozi watakaokutana ni wenyeviti wa vyama, makamu wenyeviti, makatibu na wajumbe wa sekretarieti kutoka ndani ya vyama hivyo.

Umoja huo ulioanzishwa Februari mwaka jana wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, ukiundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD kabla ya kusaini makubaliano (MoU) kwa ajili ya kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi zote kuanzia udiwani, ubunge na urais. 

Siku chache zilizopita, kamati maalumu ya Ukawa ilikamilisha kazi ya ugawaji wa majimbo 170 lakini ukawapo mvutano katika majimbo 19 ambayo vyama zaidi ya kimoja vinayataka, yakiwamo ya Segerea, Kinondoni, Kigamboni na Ukonga ya Dar es Salaam, Morogoro Mjini na mengine ya mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bara, Magdalena Sakaya alithibitisha kuwapo kwa kikao hicho na kuwa kitakuwa na ajenda ya kukusanya maoni na mapendekezo ya wanachama, kujadiliana kwa pamoja ili kufikia muafaka wa majimbo hayo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa pia alithibitisha kuwapo kwa mkutano huo.

“Mkutano utakuwapo na utafanyika Zanzibar kwa mujibu wa ratiba za Ukawa,” alisema Dk Slaa bila kutaka kuingia kwa undani.

Alipoulizwa kuhusu utata katika mgawanyo wa majimbo, Dk Slaa alisisitiza kwamba, busara pekee ndiyo itatumika kumaliza mvutano uliopo. Hata hivyo, Dk Slaa alikanusha kuwapo kwa mvutano katika majimbo 28 huku akilalamikia upotoshaji uliofanyika kwa vyombo vya habari.

 “Hizo taarifa siyo za kweli na tumekuwa na utaratibu wa kutoa tamko la pamoja, nisingependa kueleza lolote zaidi ya hapo ila tusubiri vikao vya Ukawa, ni hatari sana kutoa taarifa ambazo siyo sahihi na zisizokuwa na lengo la kujenga umoja huu,” alisema Dk Slaa.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema katika hatua za kutafuta maridhiano ya majimbo hayo, vyama vyote vinapaswa kutambua kila nafasi ya chama kilichoshiriki kwenye makubaliano ya Ukawa.

“Tukifuata kanuni nadhani kuna vyama ambavyo havitakuwa na nafasi Ukawa na haitakuwa na maana ya kuungana, kwa hivyo lazima busara itumike zaidi haiwezekani chama fulani kilazimishe kuchukua majimbo mengi kuliko kingine,” alisema Nyambabe.



Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...