2015-04-09

Chadema Moro kumuunga mkono Abood


Lengo ni kutaka taarifa za fedha zinazohusu ujenzi wa kituo cha mabasi cha Msamvu

Morogoro. Mvutano wa uendelezaji ujenzi wa kituo cha mabasi cha Msamvu mjini hapa, umeingia hatua mpya baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza maandamano kuunga mkono hatua za Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Abood kuhoji matumizi ya fedha za mradi huo. 

Mradi huo wa ujenzi wa stendi ya mabasi unaofanywa kwa ubia na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) Sh720 milioni zimeshatolewa kumlipa fidia aliyejenga ghorofa ndani ya eneo hilo.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Morogoro, James Joel alisema wanakusudia kufanya maandamano Aprili 14 .

Alisema uamuzi wa kufanya maandamano unatokana na Abood kufanya ziara ya kawaida kukagua mradi huo unaofanywa kwa ushirika na Manispaa ya Morogoro ambayo imeshindwa kutoa taarifa za matumizi hayo. 

Mwenyekiti huyo wa Chadema, alisema kuwa katika mradi huo inaonekana kuna harafu ya ufisadi miongoni mwa viongozi wa manispaa ndiyo maana wanakataa kuweka wazi taarifa za mradi huo. “Tunaomba polisi ituache, haya maandamano ni ya amani...tunataka maelezo ya hizi fedha kwa kuwa fedha ni za wananchi, wanakosa huduma muhimu kutokana na mradi huo,”

Alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, Abood alisema kinachotakiwa ni kuwekwa wazi suala la fedha za mradi huo.

Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwenendo wa Bunge na Halmashauri wa Chadema, Dk Albanie Marcossy alisema maandamano hayo ni mwendelezo wa operesheni iliyoanzishwa na Chadema ya kuelimisha jamii kuhusu matumizi mbalimbali ya fedha za Serikali.

Katibu wa Chadema, Wilaya ya Morogoro, Esther Taweta alisema chama hicho kipo kwa ajili ya kutetea masilahi ya wananchi.

Alisema fedha zilizotolewa kujenga mradi wa maendeleo hazijulikani zilipo.



Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...