Wakati mwingine kuna maswali magumu sana kuweza kuyajibu. Kwa mfano kwanini watu muhimu na wazuri hufa mapema? Kwanini watu wenye umuhimu mkubwa katika jamii huondoka ghafla tena katika wakati ambapo wapo kwenye kilele cha mafanikio yao?
Chukulia mfano Aaliyah, Tupac, Notorious BIG au Stephen Kanumba! Hili ni swali gumu sana kulijibu na hivyo mambo mengine ni ya kumwachia Mungu.
Leo ni April 7, miaka mitatu tangu kifo cha muigizaji mahiri, aliyependwa, aliyekuwa na kipaji cha hali ya juu, Kanumba.
Kifo chake kilikuwa cha kushtusha na cha ghafla. Alifariki kwa kuanguka chini alipokuwa kwenye ugomvi wa kawaida na mpenzi wake Elizabeth ‘Lulu’ Michael. Kifo chake kilifichua siri ambayo wengi tulikuwa hatufahamu – kwamba Lulu na Kanumba walikuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu.
Lulu akaingia hatiani na kukabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia. Amekaa mahabusu kwa miezi mingi kabla ya kutoka kwa dhamana na sasa ikiwa wazi kuwa kesi hiyo ni kama imeshafutwa kimya kimya.
Kanumba alifariki kipindi ambacho alikuwa kwenye kilele cha mafanikio yake. Alikuwa ametoka kuigiza filamu ya kimataifa iitwayo Devil’s Kingdom akiwa na Ramsey Noah wa Nigeria.
Jina lake lilikuwa halivumi Afrika Mashariki peke yake, bali Ghana na Nigeria walikuwa wameanza kumsikia na kukubali uwezo wake.
Kanumba alikuwa na ujasiri, mbishi na hakuogopa kujaribu. Kupitia miradi yake ya kuwashirikisha wasanii wa Nollywood, wadau wengi wa filamu barani Afrika walianza kushawishika na umahiri wa filamu za Kitanzania.
Laiti kama Mungu angemwepushia mauti, leo Kanumba angekuwa mbali sana. Hakuna shaka kuwa kwa speed aliyokuwa nayo, Hollywood ilikuwa ni kituo chake ambacho kingefuata.
Kanumba aliwapa changamoto waigizaji wenzake wa filamu nchini kwa kufanya filamu zenye story za kuvutia. Ameondoka na kuacha pengo kubwa.
Miaka mitatu baada ya kifo chake, kiwanda cha filamu nchini kimeyumba sana. Bongo movies hazipo tena midomoni mwa watu. Filamu za kibongo hazitengenezi tena mijadala vijiweni. Waigizaji wa filamu hawatengenezwi tena mada vibarazani. Kiwanda hicho hakina tena msisimko.
Kiwanda kimegeuka kuwa sehemu ya vita vya maneno, makundi na miparaganyiko. Waigizaji wazuri wameanza kukata tamaa na hali ilivyo sasa na kuamua kutafuta njia mbadala za kuendesha maisha yao.
Pamoja na kuwepo filamu nyingi sokoni, bado hazitengenezi hamu ya kuangaliwa ama kushawishi watu kuzinunua.
Tatizo kubwa ambalo kiwanda cha filamu Tanzania kinalo ni kutokuwepo na njia nzuri ya kuzifanyia promotion. Filamu nyingi zinatoka kimya kimya.
Hebu chukulia mfano huu kwamba wasambazaji wa filamu za Hollywood nchini Marekani, hutumia zaidi ya dola bilioni 4 kwa mwaka kutangaza filamu mpya kwenye TV, redioni, kwenye matangazo ya barabarani na mtandaoni.
Biashara ni matangazo, hata kama iwe biashara yenye wateja wengi kiasi gani. Kwahiyo msisimko kwenye soko la filamu za Tanzania ni mdogo sana kwakuwa wasambazaji hawatengi bajeti ya kuzitangaza filamu zao.
Kadri miaka inavyozidi kwenda, filamu za Tanzania zinaendelea kuwa za kawaida sana. Hali hii ikiendelea hivi hivi, kuna wasiwasi kuwa kiwanda hiki kitakufa kabisa!
RIP Kanumba.
0 comments:
Post a Comment