2015-04-07

Lowassa: Nafurahishwa na hali ya amani na usalama Zanzibar.


Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa amesema anafurahishwa na hali ya amani na usalama iliyopo Zanzibar.

Lowassa ambaye yupo visiwani Zanzibar kwa mapumziko ya sikukuu ya Pasaka, alitoa kauli hiyo mara baada ya kumalizika misa ya Pasaka katika Kanisa la Kikirsto la Kilutheri (KKKT) Ushirika wa Zanzibar.

Alisema viongozi wa Zanzibar wanapaswa kupongezwa kutokana na juhudi wanazochukua katika kudumisha amani na usalama, jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya jamii.

“Msingi wa amani ya nchi aliyoanzisha Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume inapaswa kulindwa na kuendelezwa kama njia moja wapo ya kumkumbuka na kumuenzi,” alisema Lowassa.

Akizungumzia kawaida yake ya kufanya ibada za sikukuu visiwani hapa kwa muda mrefu sasa, Lowassa alisema anapenda kufanya hivyo kwa lengo la kuimarisha na kusimamia misingi ya umoja na amani iliyopo nchini. 


Alisema umuhimu wa amani ni jambo linalohitajika muda wote ili kurahisisha kufanyika kwa ibada ambayo ni miongoni mwa haki za kikatiba za wananchi wa Tanzania bila ya kujali itikadi au imani zao.

“Amani inazidi kuwa muhimu kwani ni chanzo muhimu cha kufanyika kwa ibada kwani bila ya amani hata idaba hazitaweza kufanyika”, alisema Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli.

Akizungumzia kuhusu shambulio la kigaidi lilotokea katika Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya, alisema tukio hilo ni la kusikitisha na Tanzania inapaswa kuchukuwa tahadhari ili amani isiweze kutoweka. 



Akitoa mahubiri katika ibada hiyo, Kaimu Mkuu wa kanisa hilo, Benjamen Lusongo Mbilinyi aliwataka waumini na Watanzania kwa ujumla kuwa na upendo miongoni mwao kama njia ya kuimarisha maelewano miongoni mwa waumini wa dini na imani tofauti .

Naye Askofu wa Kanisa la Assembles of God Zanzibar, Dickson Kagange aliwataka waumini wa kanisa hilo kuhakikisha wanachagua viongozi bora uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kuisoma katiba inayopendekezwa ili kutoa maamuzi bila ya kushawishiwa kuikubali au kuikataa.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...