KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM,Nape Nnauye amerusha kombora kwa Chama cha Demokrasia na Maendekeo (CHADEMA) akidai makundi ya vijana wa ulinzi vya chama hicho (Red Brigade) yameandaliwa kwa ajili ya kuingia msituni kwa shughuli za ugaidi.
Kauli hiyo aliitoa juzi wilayani Mpwapwa kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, inayoendelea mkoani Dodoma.
“CHADEMA wanaandaa vijana kupitia Red Brigade ili kuingia msituni na kuchukua madaraka ya nchi kwa mabavu. Wanafanya hivyo kwa sabababu wanajua hawawezi kuchaguliwa kwa njia ya kura wakati wa uchaguzi mkuu,” alisema Nape na kuongeza:
“Hawa wanaopiga kelele huko mitaani eti Red Brigade wanaandaliwa kwa ajili ya kulinda kura, naomba niwaulize hizo kura wanazotaka kulinda nani atawapigia? Hata hizo kura za kuiba zitatoka wapi,” alisema.
Nape alidai kwamba tayari CCM wamepata taarifa nyeti za mpango ovu unaoandaliwa na CHADEMA kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwamba kuna mpango wa kuwatumia vijana wa Red Brigade.
“Taarifa tulinazo ni kwamba Red Brigade ni vikosi vinavyoandaliwa kwa ajili ya vitendo vya ugaidi na shughuli nyingine za ovyo. Taarifa ni kwamba hili ni kundi la kigaidi, wataanzishaje kundi la usalama wakati tunavyo vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi yetu?” alihoji Nape.
Nape alikituhumu pia chama hicho kwa kujihusisha na vitendo vya kuvunja amani katika matukio mbalimbali nchini ikiwamo yale yaliyotokea kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga na maeneo mengine kama Morogoro na kusababisha kuuawa kwa kijana muuza magazeti.
0 comments:
Post a Comment