Hakuna ambaye alitarajia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji mwaka huu kama ungekuwa na upinzani mkubwa kama uliotokea .
Tumeshuhudia katika uchaguzi huu, watu wakipigana hadi damu kumwagika, nyumba kuchomwa moto, masanduku ya kura kuibwa na kura kuchomwa moto na hata kukamatwa kwa baadhi ya wabunge na wanasiasa.
Uchaguzi huo uliofanyika kuanzia Desemba 14, mwaka huu, licha ya kuwa na upungufu mkubwa uliosababisha kurejewa katika maeneo kadhaa, lakini umetoa funzo kubwa kwa Watanzania na hasa vyama vya kisiasa.
Uchaguzi wa mwaka huu, tofauti na chaguzi zilizopita, umewaweka matatani wakurugenzi wa halmashauri 17, sita kati yao wakifukuzwa kazi, watano wakipewa onyo na wengine sita wakisimamishwa.
Jingine kubwa, katika uchaguzi huu, ulikuwa ni muungano wa vyama vya upinzani, kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuamua kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi mbali mbali.
Katika chaguzi zote zilizopita tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, hakukuwahi kuwa na muungano kama huu.
Ingawa mara kadhaa, viongozi wa upinzani walikuwa wakikutana na kukubaliana kuungana na kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi mbali mbali, lakini wamekuwa wakivurugana.
Safari hii, Katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, walau baadhi ya vyama vinavyounda Ukawa walikubaliana kusimamisha mgombea mmoja katika maeneo kadhaa nchini.
Licha ya mpango huu, pia kukabiliwa na vikwazo kidogo, lakini kwa kiasi kikubwa umeweza kuvinufaisha vyama vya upinzani kwa kuwaunganisha wanachama wao kupambana na wana CCM katika kura.
Vyama ambavyo viliungana kupitia ukawa ni Chadema, CUF, NLD na NCCR- Mageuzi.
Muungano huu umesababisha matokeo tofauti kubwa ya matokeo ikilinganishwa na ule wa mwaka 2009.
Takwimu zinasoma wakati mwaka 2009 CCM ilishinda vijiji 9,800, mwaka huu imeshinda vijiji 7,290 licha ya vijiji kadhaa kuongezwa katika maeneo mengi nchini.
0 comments:
Post a Comment