2014-11-24

CUF wamtaka Pinda ajiuzulu

                                     Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Chama cha Wananchi (CUF) kimemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kujiuzulu kwa kupotosha umma kuhusu fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu sakata hilo lililotokana na mkataba wa kuuziana umeme wa dharura kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Alisema kuwa Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa Serikali bungeni ambaye Mei mwaka huu aliuopotosha umma kwa kueleza kuwa fedha za Escrow zilizoibwa si za umma bali ni za wanahisa.

“Tunamtaka Waziri Mkuu awajibike kwa kitendo cha kupotosha umma, alichokifanya, kama asipojiuzulu inabidi afukuzwe kazi mara moja, amekuwa akitafuta visingizio vya kuzuia mjadala wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ndani ya Bunge ,” alisema Lipumba.

“Uwajibikaji pia umewalenga Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Msawi, hawa wote wanatakiwa kuungana na Pinda kuachia ngazi,” alisema.

Aidha, alisema Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) iwatie hatiani wamiliki wa IPTL na kuwafungulia mashtaka ya rushwa na wizi wa mali ya Tanesco huku akisisitiza isifanyike ajizi kama ilivyokuwa katika kashfa ya ununuzi wa rada ambapo wakala, Saileth Vithlani, alipelekwa mahakamani na baadaye akatoroka nchini.

Aliongeza kuwa sakata hilo limeonyesha wazi umuhimu wa Bunge kusimamia serikali na wabunge kutokuwa mawaziri kama ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji warioba, lakini baadaye mapendekezo hayo yaliondolewa na Bunge Maalum la Katiba (BMK).

Alisisitiza rasimu ya Warioba ilipendekeza zawadi za viongozi zirejeshwe serikalini, lakini taarifa za vigogo wengi kupewa fedha toka akaunti ya mmoja wa wanahisa wa IPTL zimeonyesha umuhimu wa mapendekezo ya Warioba yaliyonyofolewa na Mwenyekkiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge.

Alifafanua baada ya mjadala wa Bunge kukamilika CUF kwa kushirikiana na wadau wengine kitaandaa maandamano makubwa ya kulaani vitendo vya kifisadi kuhusiana na akaunti hiyo na kuwapongeza wabunge walioibua hoja na Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (PAC) hali iliyopelekea CAG kufanya ukaguzi.

ippmedia

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...