Wimbi la madaktari feki limezidi kushika kasi nchini baada ya daktari mwingine wa aina hiyo kukamatwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa Ubongo (Moi) Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Daktari huyo feki alikamatwa jana ikiwa imepita miezi 10 tangu kukamatwa kwa daktari mwingine feki katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro.
Daktari huyo feki ametambuliwa kwa jina la Dismas Macha (35) ambaye ni mkazi wa Upanga Magharibi, jijini Dar es Salaam na mzaliwa wa Moshi vijijini, mkoani Kilimanjaro.Alikamatwa baada ya kukutwa akihudumia wagonjwa katika moja ya wodi za taasisi hiyo. Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dk. Athuman Kiloloma, akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo na alisema mtuhumiwa alikamatwa saa 3:00 asubuhi jana akiwa amevaa sare za taasisi hiyo.
Alisema mtu huyo alikamatwa baada ya kuonekana akihudumia wagonjwa akiwa na karatasi yenye orodha ya majina ya zaidi ya watu 30, wakiwamo madaktari na wafanyakazi wa taasisi hiyo. Dk. Kiloloma alisema karatasi hiyo inaonyesha kuwa, mtu huyo alikuwa anawaomba madaktari na wafanyakazi hao mchango kwa ajili ya kupata fedha za kusafirisha mwili wa mkewe, ambaye amefia nchini India, "hili ni tatizo kwa mtu asiye na sifa kujiita daktari na kuanza kukusanya michango kutoka kwa madaktari kwa kisingizio kuwa mkewe amefariki nchini India, hivyo alikuwa akikusanya fedha ili kuwezesha mwili kurudishwa nchini" alisema Dk. Kiloloma.
Dk. Kiloloma alisema baada ya kuonekana Muhas, uongozi wa MNH ulibandika tangazo na picha ya mtu huyo iliyokuwa ilikieleza kuwa hahusiki katika hospitali hiyo, na baada ya kukamatwa na kuhojiwa awali alidai kwamba alidai kuwa alikwenda Moi kwa ajili ya kumuona mgonjwa, lakini baadaye akasema alikwenda kumuona ndugu yake ambaye ni daktari katika taasisi hiyo. Kuhusu nyaraka alizokutwa nazo, Dk. Kiloloma alisema mtu huyo alipoulizwa alisema alinunua kwa matumizi yake binafsi.
Daktari feki huyo alifikishwa katika kituo cha polisi Salender Bridge, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yake. Kamanda wa Polisi Mkoa Ilala, Mary Nzuki, hakupatika kuzungumzia tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment