2014-12-31

Lazima;Hatua zaidi zatakiwa kuchukuliwa wahusika wa ESCROW.

Wakati baadhi ya wananchi na taasisi mbalimbali nchini zikiendelea kushinikiza uwajibishwaji wa baadhi ya viongozi waliohusika na wizi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, umoja wa shirikisho la chuo kikuu cha Dodoma umeshauri hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya wahusika wote kwani kuvuliwa nyadhifa zao pekee haitoshi. 


Aidha shirikisho hilo limempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuanza kuwawajibisha baadhi yao likimshauri kuendelea pia kuwashughulikia wale wote waliobaki katika sakata hilo.

Tamko hilo lililotolewa mjini Dodoma na Rais wa shirikisho hilo Fredrick Luterano limedai kuwa mazoea yaliyojengeka hapa nchini kwa baadhi ya viongozi kuvuliwa nyadhifa zao bila hatua zaidi kuchukuliwa umekwisha na sasa umefika muda wa kuchukua hatua zaidi ili liwe fundisho kwa wengine. 


Kwa upande mwingine Rais huyo wa shirikisho la chuo kikuu cha Dodoma akatumia nafasi hiyo kuzitaka mamlaka za vyama vya siasa kuwachukulia hatua wanachama wao wanaopita mitaani wakigawa fedha na kutangaza nia ya kugombea nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwemo Urais.

Sakata la wizi wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow limechangia kujiuzuru kwa mwanasheria mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema na Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaiujka akitakiwa kujipima ambapo Katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakimu Maswi akisimamishwa kupisha uchunguzi na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Mhongo akiwekwa kiporo.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...