Iringa. Baada ya kuibuka na ushindi wa wenyeviti 65 katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema viongozi hao wanapaswa kuonyesha tofauti ya kiutendaji dhidi ya viongozi wa CCM kwa kurejesha misingi ya haki, uwajibikaji kwa watu wote watakaowasimamia.
Akizungumza jana katika Viwanja vya Mwebetogwa mjini hapa, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema ushindi huo pia ni ishara kuwa CCM haiwezi kushinda kiti cha Ubunge Iringa Mjini katika uchaguzi ujao.
“Kama tuliweza kushinda ubunge mwaka 2010 tukiwa na mwenyekiti mmoja wa mtaa, iweje tushindwe tukiwa na wenyeviti 65?” alisema.
Alisema viongozi wa Chadema watakaoshindwa kutekeleza ahadi walizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni, chama kitawanyang’anya kadi zao za uanachama.
Kuhusu masuala ya kitaifa, Msigwa alisema kwa sasa kuna ombwe la uongozi na kutumia fursa hiyo kumtaka Rais Jakaya Kikwete ambaye kesho atalihutubia Taifa, kuwachukulia hatua wahusika wote waliotajwa kuchota Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Bunge limetoa maazimio yake na ikumbukwe kuwa Bunge linafanya kwa niaba ya wananchi, sasa kwa nini maazimio ya Bunge yasitekelezwe na rais, “ alihoji Msigwa huku akiwataka walimu na polisi kuikataa Serikali ya CCM kwa maelezo kuwa haitetei masilahi ya wananchi
0 comments:
Post a Comment