2015-01-21

Afunguka;Askofu Mokiwa Tukimchagua rais kwa tamaa za rushwa itatugharimu miaka mitano


Dar es Salaam. Dakika zinaendelea kusogea na mapigo ya moyo yakizidi kwenda kasi kwa baadhi ya wanasiasa walioanzisha mbio za uchaguzi ili kurithi mikoba ya Rais Jakaya Kikwete, ubunge na udiwani, unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.


Hatua hiyo inachagizwa na kila chama cha siasa au mwanasiasa mmoja mmoja kutumia nafasi yake kujipanga vyema katika ushindani huo licha ya kuwapo na joto kali la kisiasa kupitia makundi ya wafuasi.


Hata hivyo, vijana wanaonekana kutumiwa zaidi katika masuala ya uchaguzi kama mtaji mkubwa hasa kutokana na ukweli kwamba katika wapiga kura wao ni wengi zaidi.


Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk Albina Chuwa anasema kulingana na Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2012, vijana ni asilimia 34.7 ya watu wote nchini Tanzania pia ndiyo wengi zaidi katika kundi la wale wenye umri kati ya miaka 18 hadi 100.


Kutokana na mazingira hayo, mwandishi wa gazeti hili amefanya mahoajiano na Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa ili kupata mtazamo wake juu ya hatima ya makundi ya vijana, tahadhari na maandalizi yanayohitajika katika siasa nchini.


Swali: Baba Askofu, unawezaje kuyaelezea makundi ya vijana jinsi yanavyotumika kisiasa hasa ikizingatiwa katika miaka ya karibuni wanaonekana kushabikia sana siasa.


Jibu: Ni hatari kubwa sana, hatua hiyo inatokana na kukosa mwelekeo mzuri wa maisha na ufahamu wa kutosha juu ya mustakabali wa maisha yao ya baadaye. Pia kwa kutumia udhaifu huo, mwanasiasa yeyote amekuwa na uwezo wa kumtumia kijana kama toilet paper (kitambaa cha kujifutia uchafu).


Ifahamike kwamba, nguvu ya kijana ni kulinda hali ya nchi na siyo kulinda itikadi za vyama. Athari zake inaweza kusababisha vijana hao hao kesho watawageuka na kubebea mapanga kwa sababu hawatakuwa wamepata suluhu ya mahitaji yao.


Changamoto zao kama vile elimu, afya, zimewekwa kando bila wao kujijua na badala yake wamekuwa wakitumika kama chombo cha kufanikisha maslahi ya wanasiasa hao, ni hatari sana kutengeneza makundi kwa jambo lisilokuwa na msaada wa maisha yao.


Mambo ya msingi ambayo yanatakiwa kuwaunganisha vijana hao kuwa ni vita ya kuzuia wimbi la matumizi na biashara ya dawa za kulevya, magonjwa yasiyotibika, hatima ya matumizi ya ardhi yao, amani ya taifa na mahitaji muhimu kwa jamii zao lakini hatuoni hivyo. Hali itakuwa mbaya sana endapo hawatakuwa makini kule tunakoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.


Swali: Rais ajaye anapaswa kuwa wa namna gani?


Jibu: Kwa kuangalia uwezo na sifa za mgombea mwenyewe. Rais mwenye nafasi kubwa ya kupewa ridhaa na Watanzania ni yule atakayekuwa na sifa za kushughulikia changamoto sugu zinazoendelea kulitesa taifa mpaka sasa.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...