2015-01-21

Hatari;Mkulima anaswa na risasi 271 za SMG



Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP.Thobias Sedoyeka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake. 


Na Nathaniel Limu, Singida

JESHI la polisi mkoa wa Singida linamshikilia mkulima na mkazi wa Matele-Kasulu mkoani Kigoma,Discon Bavumbi Masombo Kiyungu (45) kwa tuhuma ya kumiliki risasi 271 za bunduki ya kijeshi aina ya SMG kinyume na sheria.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP.Thobias Sedoyeka, alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa Januari 18 mwaka huu huko Majengo Manyoni mjini.

Alisema mafanikio hayo ya kumkamata mtuhumiwa yametokana na taarifa sahihi zilizotolewa na raia wema kuwa mtuhumiwa alikuwa akisafirisha risasi hizo kutoka Singida mjini na kuzipeleka Manyoni mjini.

Kamanda huyo alisema baada ya taarifa hiyo,askari polisi waliweka mtego katika kituo cha mabasi kilichopo Majengo mjini Manyoni na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa baada ya kushuka kwenye gari aina ya noah. 


“Baada ya kukamatwa na kupekuliwa,aliweza kupatikana na risasi hizo ambazo alikuwa amezificha ndani ya sanduku (briefcase) lake”,alisema.

Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa ni jangili na husafirisha risasi kutoka nchi jirani ya Burundi na kuzipeleka porini kwa ajili ya kuwindia Tembo.

Imebainika pia kuwa mtuhumiwa alikuwa na wenzake ambao hawakuweza kubainika kwa majina na makazi waliofika katika kituo hicho cha mabasi kwa ajili ya kumpokea lakini walipobaini kuwa mwenzao amekamatwa,walitoroka na kukimbilia kusiko julikana.

Kamanda Sedoyeka alisema kuwa mtuhumiwa huyo bado anaendelea kuhojiwa ili kujua mahali ilipo bunduki ambayo hutumia risasi hizo ikiwa ni pamoja na kujua mtandao mzima wa ujangiri na kuwatafuta watuhumiwa waliotoroka kwa lengo la kuharibu na kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinaharibu rasilimali ya taifa.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...