2015-01-14

Inasikitisha sana:Mfanyabiashara auawa, mwingine ajeruhiwa Bunda.

 Mfanyabiashara mmoja wa kuuza samaki ameuawa kwa kupigwa risasi na mtu mwingine kujeruhiwa kwa kupigwa risasi katika matukio mawili tofauti yaliyotokea wilayani Bunda mkoani Mara.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Mara Philpo Kalangi tukio la kwanza lilitokea Januari 12 mwaka huu majira ya saa 3 usiku katika eneo la Nyasura mjini Bunda ambapo mfanyabiashara huyo akiwa na mke wake wakati wakirejea nyumbani alipigwa risasi na watu wasiofahamika ambao hawakupora kitu chochote.

Kilangi amesema ofisi yake imetuma makachero katika Wilaya ya Bunda kufanya uchunguzi wa kina juu ya matukio hayo. 


Mfanyabiashara aliyeuawa kwa kupigwa risasi ametambuliwa kwa jina la Mkome Marwa (39) mkazi wa mtaa wa Nyasura mjini Bunda ambaye alipoteza maisha usiku huo huo wakati akipatiwwa matibabu katika hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza.

Awali, baada ya kupigwa risasi mfanyabiashara huyo pamoja na mke wake walikimbilia katika mji wa jirani ambapo mwenye mji huo alifunga geti lakini mtu huyo alilipiga teke na kukuta limefungwa na kisha akatokomea kusikojulikana bila kuchukua kitu chochote.

Aidha, tukio la pili limetokea usiku huo huo majira ya saa 4:00 katika eneo la Bunda Day ambapo mwanaume mmoja Ndaro Malemi (25) aliyekuwa anakwenda nyumbani kwake amejeruhiwa kwa kupigwa risasi na mtu asiyefahamika ambaye pia hakuchukua kitu chochote. 


Akisimulia mkasa huo majeruhi huyo akiwa katika hospitali ya DDH-Bunda amesema mwanaume huyo aliyekuwa amevaa koti jeusi alimvizia njiani na kumwamuru atoe kila kitu na kwamba baada ya kukimbia ndipo alipompiga risasi mbili na yeye akatokomea kusikojulikana.

Muuguzi wa zamu katika wodi ya wanaume katika hospitali ya DDH-Bunda Sesilia Mbuya amesema hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri.

Polisi wamesema wanakisia silaha iliyotumika katika matukio yote mawili ni Bastora kulingana na maganda ya risasi yaliyookotwa kwenye maeneo ya matukio hayo na kwamba hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na upelelezi bado unaendelea.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...