2015-01-05

Kila chenye Mwanzo Kina Mwisho; Panya Road 36 mbaroni

JESHI la Polisi nchini linawashikilia vijana 36 wanaotuhumiwa kujihusisha na kikundi cha uhalifu jijini Dar es Salaam, maarufu kama ‘panya road’, ambacho kilizua taharuki kubwa juzi.
 
Vijana wa kikundi hicho wenye umri wa kati ya miaka 16 mpaka 30, walizua vurugu katika maeneo mbalimbali ya jiji na kusababisha baadhi ya shughuli kusitishwa kwa muda.

Wananchi walikuwa na hofu ya kuvamiwa na wahalifu wa kikundi hicho, waliokuwa wanapiga watu, kupora na kuharibu magari.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema chanzo cha taharuki hiyo, ilitokana na kuuawa kwa mtu mmoja, Mohamed Ayub na wananchi waliojichukulia sheria mkononi.

Alisema kijana huyo aliuawa na wananchi kwenye mkesha wa sikukuu ya Mwaka Mpya kwa tuhuma za wizi katika eneo la Tandale Kwa Mtogole.

Baada ya kijana huyo kuuawa, maziko yake yalifanyika juzi saa 9:00 jioni katika makaburi ya Kihatu, Magomeni Kagera, ambapo polisi ilipata taarifa kuwa vijana wenzake walijipanga kufanya fujo.

“Polisi ilipata taarifa kuwa baada ya maziko hayo, vijana wenzake walikuwa wamejipanga kufanya fujo ili kulipiza kisasi cha mwenzao kuuawa, lakini kabla ya vurugu hizo kufanyika, polisi walikuwa wameona dalili na waliweza kuzidhibiti,” alisema Bulimba.

Akifafanua jinsi taharuki ilivyoanza, alisema baada ya polisi kufanikiwa kudhibiti vurugu hizo kwa kupiga mabomu ya machozi kutokana na vijana hao kuwa kundi kubwa, walianza kutawanyika kwa kukimbilia katika maeneo mbalimbali na kuzua taharuki hiyo kwa wananchi, kwamba huenda wanapokimbilia wana mpango wa kufanya fujo.

Alisema kutokana na taharuki hiyo, polisi inaendelea na msako wa kuwabaini na kuwakamata wote wanaojihusisha na uhalifu na kuzua hofu kwa wananchi na kusababisha washindwe kufanya shughuli zao za maendeleo.

Aliwataka wananchi kutokuwa na hofu na kuwataka waendelee na shughuli zao kama kawaida.

“Mpaka sasa tunawashikilia vijana hao 36 kwa mahojiano na uchunguzi zaidi ili watusaidie kutuonesha wenzao na kwa nini wanafanya uhalifu wa aina hii, uchunguzi utakapokamilika tutawafikisha mahakamani,” alisema Bulimba.

Aidha, alisema jeshi hilo linatoa onyo kwa vijana wanaojihusisha na vikundi hivyo, kuacha tabia hiyo. Alisema jeshi la Polisi limejipanga vizuri, kuhakikisha kuwa linadhibiti vikundi vya uhalifu na vinatokomezwa.

“Pia tunachunguza kama kuna mtu ambaye yuko nyuma ya vikundi kama hivi, kwa sababu hawa ni watoto wadogo sana, kwa hiyo hilo nalo tunalifuatilia ili kubaini, tunataka kuhakikisha nchi inaongozwa kwa kufuata sheria, hatutamwonea muhali mtu au kikundi chochote kinachotaka kuvuruga amani ya nchi,” alisema.

Juzi katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, shughuli zilisimama kwa muda kutokana na taharuki hiyo, ambapo maduka yalifungwa na hata usafiri wa daladala kuwa wa shida, kutokana na wananchi kuhofia usalama wao.

Taharuki

Taharuki hiyo ilitawala kwa zaidi ya saa nne kuanzia alasiri. Hata hivyo, taarifa za kuwepo kwa kikundi hicho ziliongezewa chumvi na hivyo kuongeza hofu miongoni mwa wananchi wa maeneo mbalimbali.

Taarifa hizo zilizokuwa zikisambazwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ya Facebook, Twitter, Jamii Forum, Instagram, Whatsapp na ujumbe wa kawaida, zilieleza kuwa kikundi hicho kilikuwa kikifanya vurugu na uporaji kwa kuhama eneo moja kwenda jingine.

Taarifa hizo zilidai kikundi hicho kilifanya vurugu na uporaji katika maeneo ya Mwenge, Sinza, Kinondoni, Magomeni Kagera, Mwananyamala, Manzese, Tandale Kwa Tumbo, Kigogo, Buguruni, Ubungo, Mwenge, Mabibo na Tabata na maeneo mengine.

Makundi hayo kipindi cha nyuma

Vikundi vya uhalifu wa aina hiyo, vimekuwa vikiibuka na kupotea mara kwa mara. Vikundi hivyo ni mbwa mwitu, watoto wa mbwa, waasi na panya road. Makundi mengine ya kihalifu yaliyowahi kujitokeza ni komando yosso na kiboko msheli.

Katika kipindi cha Mei mwaka jana, kikundi hicho cha panya road kilizuka na kuibua tafrani kubwa miongoni mwa wananchi wa maeneo mbalimbali, ambapo walikuwa wakiwavamia mitaa wakiwa na silaha za jadi mbalimbali kama nondo, mawe, visu, mapanga na kuwashambulia wananchi.

Katika kipindi hicho, Polisi iliwaagiza makamanda wake wa mikoa ya kipolisi ya Kinondoni, Ilala na Temeke kutokomeza vikundi hivyo. Agizo hilo lilitolewa na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki.

Baada ya agizo hilo kutolewa, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema walifanikiwa kukamata baadhi ya viongozi wa makundi ya mbwa mwitu na panya road na wafuasi zaidi ya 100. Viongozi wa mbwa mwitu walifikishwa mahakamani.

Baada ya msako huo kufanywa na Polisi, makundi hayo yalipotea kwa muda. Lakini, panya road waliibuka tena Novemba mwaka jana, ambapo walifunga mitaa minne ya Tabata na kusimamisha shughuli za mitaa hiyo, kutokana na kile kinachodaiwa kulipa kisasi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...