2015-01-14

MAMBO HAYO;HONGERA KINGUNGE.



Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale - Mwiru jana aliripotiwa kwenye gazeti hili akidai kuwa wote waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hawana sifa kwa kuwa wanatumia fedha kutaka kuingia Ikulu.

Kingunge alisema: “Kuna suala la kukosa uadilifu, kuna suala la matumizi ya pesa na nikwambie ukweli, hao wanaotangaza urais wote wanatumia pesa, wanatumia faulo mbalimbali na wananchi wanajua.”


Bila kutaja majina, Kingunge alisema makada hao wamekuwa wakitumia fedha nyingi kujitangaza na kutengeneza ushawishi wa kukubalika kwa wananchi jambo ambalo ni kinyume na maadili ya uongozi.


Mimi namuunga mkono mzee wetu Kingungwe na ningependa kuona Watanzania wanawachambua wote wanaoonyesha nia ya kugombea ili kuwafumbua macho Watanzania.


Siamini kabisa kama Mzee Kingunge ameyasema hayo pengine kwa lengo la kuwaharibia hawa ambao tayari wameonyesha nia ili kumpa nafasi mtu wake.


Kingunge amethubutu kusema kuwa wote waliotangaza nia “hakuna msafi hata mmoja”. Watu wengine wenye upeo nao wajitokeze waseme wazi fulani hafai. Hakuna haja ya kuoneana aibu. Ningependa kuona wasomi katika nchi hii wakiwachambua wale wote waliotangaza nia kuanzia mienendo yao, utendaji wao wa kazi na hata upeo wao katika kuchanganua mambo. Jambo hili lisifanywe kwa fitina au uchochezi.


Maana ukumbi kama huo unaweza kutumiwa pia na watu waliopandikizwa kwa lengo la kuwatibulia wapinzani wao. Mijadala yenye nia ya kweli ya kutoa mustakabali wa nchi yetu ipewe nafasi.


Watanzania tukithubutu tunaweza. Awamu ya Tano tunataka Rais anayejua matatizo ya Watanzania si kumchagua kwa kuangalia chama, ukabila, udini, uzuri wa sura, uwezo wa kifedha, ucheshi au kwa kigezo tu hana kashfa.


Lazima awe anajua kwa undani matatizo ya Watanzania. Anayejua nini kimesababisha nchi hii kuendelea kuwa maskini wakati tunazo rasilimali nyingi kama vile madini, gesi, ardhi nzuri yenye rutuba na kadhalika. Kilimo kinakufa, watu wanakimbia vijijini, wanatafuta maisha mijini.


Tunataka rais atakayesimama imara na kukemea viongozi wasio waadilifu, wazembe, mafisadi na wenye kufanya kazi kwa mazoea bila ubunifu.


Watanzania wangependa kuona Tanzania inasifika kwa uuzaji wa madini ya Tanzanite ambayo hayapatikani sehemu nyingine yoyote duniani. Maana tunajiuliza Kenya na India kusifika kwa uuzaji wa Tanzanite kwenye soko la dunia, hii inakuwaje? Maana hili haliingii kabisa akilini.


Tanzania tuna madini mengi yanayochimbwa na kuuzwa kwa mabilioni ya fedha soko la kimataifa lakini ukiangalia hali za wananchi wamedhoofu. Choka mbaya! Tatizo nini?

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...