HOMA ya Uchaguzi Mkuu 2015 inazidi kupanda. Wapo baadhi ya wagombea wa urais ambao tayari wameshatangaza nia hadharani lakini wengine wanaendeleza harakati zao chini kwa chini.
Miongoni mwa makada ambao tayari wameonesha nia ya kutaka kugombea ni pamoja na vijana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (40) na Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba (41).
Mwigulu ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi mkoani Singida, amekuwa na mvuto wa aina yake kisiasa huku akionekana kupendwa zaidi kutokana na kujiwekea nembo yake kwenye mavazi anayovaa kwa kujifunga skafu ya bendera ya taifa.
Mbali na mvuto, Mwigulu tayari alishaanza mizunguko katika majimbo mbalimbali nchini na kuanza kupiga kampeni za ‘kiaina’ ambapo ameonekana kukubalika katika maeneo mbalimbali aliyopita ikiwemo Tanga na Morogoro kabla ya kupigwa ‘stop’ na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Kuonesha kwamba amejipanga, Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, alizua gumzo zaidi alipokuwa akitumia usafiri wa helkopta katika ziara zake ambazo zilikuwa zikitoa taswira kwamba kweli anakubalika na wengi.
Kwa upande wake Makamba, Mbunge wa Bumbuli, alionesha nia mapema na kuwafanya vijana wengi wampe sapoti katika harakati zake za urais.
Umaarufu wa Makamba pia unachagizwa zaidi ya umaarufu na misimamo aliyokuwa nayo baba yake, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba ambaye alikuwa akifanya mambo mengi ya maendeleo na kukemea matatizo mbalimbali nchini.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (40).
Mbali na mvuto wa uongozi, Makamba amezua gumzo zaidi baada ya kutoa kitabu chake ambacho kinaelezea mikakati ya kuwania nafasi ya urais.
Mwigulu na Makamba wanazua msuguano mzito kutokana na kigezo cha ujana ambacho kinawabeba, hali ambayo imewafanya wananchi wanaoamini katika falsafa ya viongozi vijana kushindwa kupata jibu la moja kwa moja juu ya nani atapendeza kupitishwa na chama.
Ukiachana na kigezo hicho, vijana hao ni wasomi. Mwigulu ana ya Shahada ya Uzamili ya Uchumi, Shahada ya Uchumi na Cheti cha Uongozi ambapo masomo yake amehitimu Chuo Kikuu cha Dar.
Makamba yeye ana Shahada ya Uzamili ya Diplomasia na Usuluhishi wa Migogoro, Shahada ya Diplomasia na Usuluhishi wa Migogoro ambazo amehitimishia katika Chuo cha George Mason, Marekani.
Wote wawili wana uzoefu mkubwa ndani ya chama. Mwigulu kabla ya kuwa Naibu Waziri wa Fedha mwaka jana, amekitumikia chama tangu hatua ya mkoa, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Umoja wa Vijana (UV-CCM) nafasi ambazo anazitumikia hadi sasa.
Makamba naye vivyo hivyo, ana uzoefu wa kutosha chamani kuanzia ngazi ya afisa wa mambo ya nje chini ya Rais Jakaya Kikwete ambaye pia alizunguka naye nchi nzima katika kampeni zake mwaka 2005.
Swali la kwamba nani ataibuka kidedea kuwakilisha nafasi ya ugombea kupitia chama chao ndilo ambalo linaleta utata kutokana na sifa za kila mmoja, tusikilizie hadi Machi, mwaka huu pale atakapotangazwa rasmi.
0 comments:
Post a Comment