Ni katika ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vimepata hati zenye mashaka katika ukaguzi wa hesabu zake, uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Juni 2013.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyopatikana jijini Dar es Salaam jana, CAG ameainisha vigezo saba tofauti vilivyosababisha hesabu za CCM kupata hati yenye mashaka na kueleza kuwa CCM imekosa uhalali wa kisheria kumiliki baadhi ya mali ilizonazo.
Upande wa Chadema, CAG ameanisha vigezo vitatu vya kupata hati hiyo na kubainisha kuwa zaidi ya Sh500 milioni zilitumika na chama hicho kununulia magari kumi bila kuidhinishwa na bodi ya zabuni.
Ukaguzi huo wa CAG umefanyika kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1992 ya Vyama vya Siasa, iliyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 7 ya mwaka 2009, inayompa CAG mamlaka ya kukagua hesabu za vyama vya siasa.
“Naamini ushahidi niliopata unatosha na sahihi kutoa maoni kuhusu ukaguzi wangu,” ilisema sehemu ya taarifa ya CAG kwa mwaka 2012/13 kwa vyama hivyo na kuongeza:
“...CCM haikutenganisha thamani ya ardhi na nyumba vilivyo na thamani ya Sh11, 422,576,990.52. Hatukuweza kupata taarifa ya fedha ya CCM iliyokaguliwa kuhusu rasilimali zake zinazofikia Sh9,632,576,701.57.”
Ilibainisha vigezo vingine vya hati yenye mashaka kuwa ni CCM kutowasilisha taarifa ya mapato yake ya fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali zilizofikia Sh1,526,536,802, huku CAG pia akishindwa kupata nyaraka za kuthibitisha matumizi na malipo yaliyofanywa na chama hicho yanayofikia Sh6,045,438,052.
Hata hivyo, mwaka jana CCM kilitangaza kuwa CAG, amekamilisha ukaguzi wa hesabu za chama hicho zilizoishia Juni mwaka 2012/13.
CCM ilieleza kuwa ukaguzi huo ulikuwa wa hesabu zilizoishia Juni 30, 2013 na ulifanywa kuanzia Mei 19, 2014 mpaka Oktoba 2014 na kueleza kuwa imekuwa ikikagua hesabu zake kwa wakati kila mwaka bila kutoa wito kwa CAG kutosita kutoa taarifa kwa umma inapotokea chama cha siasa hakitoi ushirikiano katika kutimiza matakwa ya ukaguzi kisheria.
Kwa upande wa Chadema, taarifa hiyo ya CAG ilisema: “Katika ukaguzi tulibaini kwamba Chadema ina zaidi ya akaunti 200 katika benki mbalimbali nchini lakini fedha zilizotajwa kuwapo katika taarifa zake katika mwaka ulioishia Juni 2013 ni Sh224,824.750.56 kati ya hizo Sh221,060,446.41 zikiwa ni salio katika akaunti zake sita na kuacha salio la Sh3,764,304.15 kwa akaunti zaidi ya 194 zilizosalia:
Magari 10 yalinunuliwa kwa Sh559,031,330 bila kuidhinishwa. Sh27,500,000 zilitumika kukodi jenereta bila kuwa na nyaraka zinazohalalisha matumizi yake.”
Taarifa hiyo ya CAG ilieleza kuwa katika vitabu vya risiti vya Chadema pia ilishindwa kuwasilisha kwa ukaguzi kitabu cha risiti chenye namba 451-500 kilichotumika kukusanya Sh30,163,152 hivyo kuzuia kufanyika kwa ukaguzi.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment