2015-03-18

Ufisadi CCM, Chadema


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameibua ufujaji wa mabilioni ya fedha kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika ripoti ya ukaguzi wa CAG kwa vyama hivyo aliyoikamilisha Septemba mwaka jana kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa namba tano ya mwaka 1992, sehemu ya 14 (1)(b) imeibua madudu hayo.

Taarifa hiyo ya CAG ambayo MTANZANIA imeiona, imechambua hesabu za Chadema na CCM na kusema wakati wa ukaguzi walibaini masuala mengi ikiwamo kutotolewa taarifa sahihi za matumizi.

HESABU ZA CCM
Kutokana na hali hiyo, CAG alilazimika kutoa hati yenye shaka kwa chama tawala – CCM ambacho kilionyesha kumiliki mali za kiasi cha Sh bilioni 19.5.

Hata hivyo, imebainika kuwa CCM haina daftari la mali za kudumu (Fixed Assets Register), ambalo lingeweza kubainisha ukamilifu wa taarifa kuhusu umiliki huo wa fedha za chama hicho.

CAG alisema chama hicho hakikufanya tathmini ya mali zake kwa kipindi kirefu, hivyo, fedha hizo haziwakilishi thamani halisi.

Alisema chama hakikutenganisha thamani ya ardhi na majengo badala yake kikieleza kuwa na thamani ya Sh bilioni 11.4 ambapo alishindwa kubainisha kwa kutenganisha thamani za ardhi na zile za majengo kama kinavyoagiza kifungu cha 58 cha viwango vya uhasibu vya kimataifa (IAS) 16.

“Hatukuweza kupata taarifa za ukaguzi zinazounga mkono uwekezaji wa CCM ulioelezwa kuwa na thamani ya Sh bilioni 9.6 ambao umejumuishwa katika hali ya taarifa ya kifedha iliyoishia Juni 30, 2013 zilizoelezwa katika vipengele 6 na 7 vya taarifa za fedha. Wala hatukuweza kujiridhisha kiwango cha fedha kinachobeba uwekezaji huo katika makampuni yaliyotajwa.

“Pamoja na matumizi na malipo kwa taasisi zinazohusiana na chama yenye thamani ya shilingi bilioni 3,576,906,142 kama yalivyoelezwa katika kipengele 21 cha taarifa ya fedha iliyoishia Juni 30, 2013. 
Tulibaini taasisi za chama hazikuandaa wala kuwasilisha taarifa za fedha kwa ajili ya ukaguzi na hata kuthibitisha matokeo ya usimamizi wa rasilimali zilizokabidhiwa mikononi mwao,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza:

“Chama hakikuripoti vyema ruzuku ilizopatiwa na wafadhili mbalimbali kama inavyoagizwa na misingi ya kihasibu. Hilo lilisababisha upungufu wa maelezo kuhusu shilingi bilioni 1.5 za ruzuku zilizoripotiwa.”

Mbali na hilo, pia imebainika katika ukaguzi huo kuwa matumizi kwa mwaka yalihusisha malipo bila kuambatanisha ushahidi wowote na kuongeza Sh bilioni 6.05 zisizo na maelezo na hivyo kutoweza kubainisha usahihi wa matumizi ya fedha za CCM.

“Ni pamoja na malipo kwa ajili ya matumizi yanayofikia Sh bilioni 7.09 yaliyoelezwa katika kipengele 18 cha taarifa ya fedha ambayo ni madeni ambayo hayajatatuliwa na hakukuambatanishwa nyaraka za upande wa tatu.
 Hakukuwa na taratibu mbadala ambazo ningeweza kupata ushahidi wa kiukaguzi kuhusu uhalali wa madeni hayo,” alisema.

HATI YENYE SHAKA
Alisema kwa mtazamo wake isipokuwa tu kwa masuala yaliyoelezwa juu ya msingi wa hati yenye shaka, taarifa za fedha ziliwasilishwa vyema, katika nyaraka zote kwa mujibu wa hali ya kifedha ya CCM kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2014 na ufanisi na mtiririko wa fedha kipindi hicho ulienda kwa mujibu wa viwango vya uhasibu vya kimataifa (IFRS).

CAG alisema baadhi ya mali zinazomilikiwa na CCM zilikosa uhalali wa kisheria wa umiliki ambazo pamoja na vipande vya ardhi, magari na uwekezaji ambao umeingizwa na kusajiliwa kwa majina ya watu binafsi.

HESABU ZA CHADEMA
Katika ukaguzi wake huo, CAG ameibaini kwamba Chadema ina akaunti zaidi ya 200 katika benki mbalimbali nchini, lakini kiwango kilichoripotiwa kama salio la kibenki na lile la matumizi madogo madogo katika taarifa za fedha kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2013 zilikuwa Sh milioni 224.8

Alisema kati ya hizo, Sh milioni 221.06 ziliwakilisha salio la akaunti za benki sita tu ikiacha salio la Sh milioni 3.7 kwa zaidi ya akaunti 194 zilizobakia.

Kutokana na hali hiyo, taarifa hiyo ya CAG ilieleza kuwa haikuweza kuthibitisha kiwango halisi cha fedha kinachoshikiliwa na Chadema kufikia Juni 30, 2013.

“Kitabu kimoja cha risiti chenye namba 451-500 ambacho kilikusanya Sh milioni 30.1 kama zilivyobainishwa katika kitabu hicho, hakikuwakilishwa kwa ukaguzi na hivyo kushindwa kupanua wigo wa ukaguzi kwa vile hatukuweza kuthibitisha kiwango sahihi cha fedha kilichokusanywa na kitabu cha risiti,” taarifa hiyo ilisema na kuongeza:

“Chadema ilionyesha umiliki wa fedha (non-current Assets) wa thamani ya Sh milioni 942.4. Hata hivyo, chama hicho hakina daftari la mali za kudumu (Fixed Assets Register), hivyo sikuweza kubainisha ukamilifu wa taarifa iliyowasilishwa kuhusiana na mali za kudumu za chama hicho,” alisema CAG katika taarifa yake

HATI YENYE SHAKA
CAG alisema kwa mtazamo wake na maelezo yaliyotolewa msingi wa hati yenye shaka, taarifa za fedha ziliwasilishwa vyema, katika nyaraka zote kufuatana na hali ya kifedha ya Chadema, kufikia Juni 30, 2014 na ufanisi na mtiririko wa fedha kipindi hicho ulienda kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya ripoti za kifedha (IFRS).

MASUALA MENGINE YENYE SHAKA
Alisema masuala mengi yenye shaka ni ununuzi wa magari 10 yaliyonunuliwa kwa Sh milioni 559.03 bila kuhusisha kamati ndogo ya chama inayohusika na zabuni huku Sh milioni 27,500,000 zilitumika kununulia jenereta.

“Hata hivyo hakukuwa na ushahidi kuonyesha kwamba mchakato wa ununuzi ulikuwa wa kiushindani kama inavyoagizwa na mwongozo wa fedha wa chama hicho,” alisema taarifa hiyo ya CAG

Alisema chama kililipa Sh milioni 47. 9 kununulia vifaa mbalimbali kwa tarehe tofauti kuanzia Novemba 2011 hadi Januari 2013.

Hata hivyo, hadi kufikia kipindi cha ukaguzi Januari 2014 vifaa vilivyolipiwa fedha hizo havikupokewa kwenye chama jambo ambalo ni kinyume na taratibu.

KAULI YA MSAJILI
Akizungumza hesabu hizo, Msajili wa Vyama Vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi, alisema kuwa ofisi yake inaandaa hesabu hizo ili ziweze kutolewa kwa umma.

Alisema kwa sasa taarifa hiyo ya ukaguzi ipo kwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali na inachapishwa ili iweze kutolewa kwa kila chama na pamoja na wanachama wao.

“Tayari tumepokea hesabu za vyama vya siasa ambazo tumezipitia na kuzipeleka wizarani ili na wenyewe waweze kuzipitia, walipomaliza wamezipeleka kwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali,” alisema

ZITTO NA RUZUKU
Oktoba 20, mwaka 2013, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, aliibua mjadala mzito kuhusu ruzuku ndani ya vyama vya siasa ambapo aliitaka Ofisi ya CAG kuchunguza uzembe wa kushindwa kukagua hesabu za vyama vya siasa kwa muda wa miaka mitatu.

Alisema CAG ameshindwa kukagua ruzuku ya Sh bilioni 83 iliyotolewa kwa vyama vya siasa nchini tangu mwaka 2005 hadi 2010.

Zitto alisema ingawa kuna tatizo katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, CAG hawezi kumtupia mzigo huo peke yake kwani naye anahusika.

“Ruzuku ya vyama vya siasa ni eneo ambalo huwa haliangaliwi kabisa, na fedha nyingi za walipakodi zinakwenda katika vyama. Kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 Sh bilioni 83 zimetolewa kama ruzuku kwa vyama vya siasa,” alisema Zitto.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...