Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya aliyewahi kugombea nafasi ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, hivi karibuni alitimiza miaka 65 na katika kuadhimisha siku hiyo, wajukuu zake walimfanyia bonge la sapraizi, Ijumaa limetonywa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya akifanyiwa 'bethidei saparaizi' na wajukuu zake.
Kwa mujibu wa chanzo chetu ambacho ni rafiki wa familia ya mheshimiwa huyo anayetajwatajwa pia kuwa mwaka huu atajitosa tena, bethidei hiyo isiyokuwa na mbwembwe ilifanyika kijijini kwake, Lufilyo, Busokele wilayani Rungwe mkoani Mbeya ambapo wajukuu zake hao walifanya tukio hilo la aina yake.
“Wale wajukuu zake walimfanyia kitu kizuri cha kuonesha wanavyompenda, walimuandalia keki ya kipekee na kisha wakampa kadi waliyoandika kwa mkono iliyosomeka ‘Happy 65th birthday’ babu.
” Utofauti wa keki hiyo ni kwamba haikuwa na mbwembwe zozote na kuonesha kuwa iliandaliwa na watoto, pembeni mwa sahani kulikuwa na kalimati zilizopangwa vizuri hivyo kuifanya iwe gumzo kwa walioiyona.
“Kilikuwa ni kitu simpo lakini cha kupendeza, mheshimiwa akakata keki pale, mambo yakaenda vizuri kabisa. Unajua kwa mheshimiwa kama yule kufanyiwa kitu kama kile kinampa faraja kubwa kuliko hata kama angeenda kufanyiwa bonge la pati ukumbini,” alisema mtoa habari huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji wa familia.
Ikaelezwa kuwa baada ya mheshimiwa Mwandosya kufanyiwa kasherehe hako, mapichapicha yalipigwa na mambo mengine kuendelea.
Ijumaa lilifanya jitihada za kumtafuta mheshimiwa Mwandosya kuzungumzia alivyojisikia siku hiyo lakini kwa bahati mbaya hakuweza kupatikana.
0 comments:
Post a Comment