2015-02-10

Hapatoshi Mbowe: Chadema haitaibiwa kura


Na Debora Sanja, Dodoma
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema chama chake hakipo tayari kuibiwa kura katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Mbowe alitoa kauli hiyo mjini Dodoma juzi, wakati akizindua mafunzo ya kikosi cha ulinzi na usalama cha chama hicho, Red Brigade, kwa vijana 200 kutoka Kanda ya Kati na kikosi maalumu kilichofuzu mafunzo ya karate.

Alisema chama hicho katika uchaguzi ujao, hakitaki kulalamika tena kwamba kimeibiwa kura.

Mbowe alisema watahakikisha wanaomba kura kwa wananchi nchi nzima na watazilinda kwa nguvu zote.
“Mwaka huu hatutaki Chadema tulalamike tena eti tumeibiwa kura, tukiibiwa kura maana yake hatupo tayari kuongoza, tutawaomba wananchi kura na tutahikikisha tunazilinda,” alisema Mbowe.

Aliwataka vijana hao kutokilinda chama peke yake, bali wawe chachu ya ulinzi kwa jamii inayowazunguka katika maeneo yao.

“Chadema itaendelea kutoa mafunzo ya ulinzi kwa vijana nchi nzima… kazi ya kupiga vita ufisadi haitawezekana kama hatutakuwa na uzalendo, tunawaandaa vijana hawa kwa ajili ya ulinzi wa chama na kuwa viongozi wa baadaye,” alisema Mbowe.

Alisema vijana hao, lazima wajenge moyo wa kujitolea, na kwamba chama hicho kilijengwa na watu wenye moyo ambao baadhi walipata madhara mbalimbali, ikiwamo kupoteza maisha.

“Jengeni sifa ya kuwa wakombozi wa taifa hili, malipo mengine siyo lazima mlipwe hapa duniani, mtayapata kwa Mungu,” alisema.

Awali akisoma risala kwa niaba ya kikosi hicho, mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Anatoly Isidory, alisema kikosi hicho kinachojumuisha mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, kina jumla ya vijana 4,271.

Alisema kati ya hao, 200 wamepewa mafunzo maalumu yatakayowawezesha kulinda chama na mali zake, viongozi pamoja na kura katika Uchaguzi Mkuu.

“Hadi sasa yapo mafanikio mengi ambayo tumeyapata, ikiwamo kulinda mikutano ya chama pamoja na kuwalinda viongozi wetu katika mikutano hiyo,” alisema Isidory.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2010, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilimtangaza Rais Jakaya Kikwete wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mshindi baada ya kupata kura milioni 5.27 ambazo ni sawa na asilimia 61.17.

Rais Kikwete alifuatiwa na mgombea wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, aliyepata kura milioni 2.27 ambazo ni sawa na asilimia 26.34.

Wagombea wengine na asilimia zao kwenye mabano walikuwa ni Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF (8), Hashim Rungwe wa NCCR-Mageuzi (0.31), Mugaywa Mutamwega wa TLP (0.20) na Peter Mziray wa APPT-Maendeleo (1.12).

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...