2015-02-03

JK aanza kukabidhi----nje ya nchi

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amekabidhi madaraka ya Uratibu wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika ya Mazingira (CAHOSCC) kwa Rais wa Misri, Jenerali Abdel Fatteh El Sisi.

Rais Kikwete alibeba jukumu la uratibu wa CAHOSCC miaka miwili iliyopita baada ya kifo cha aliyekuwa mratibu wa kamati hiyo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu, Rais Kikwete alikabidhi jukumu hilo Januari 31 na kuwatahadharisha viongozi wa Afrika juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi katika sekta ya kilimo Afrika.


Taarifa hiyo inaeleza kuwa Kikwete aliwapongeza viongozi wengine wa Afrika wakati wa mkutano wa 24 wa Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa kwa kupata mafanikio wakati wa uongozi wake.


Rais Kikwete alibainisha changamoto mbalimbali zinazolikabili Bara la Afrika kwenye mabadiliko ya tabianchi na kutaka ushirikiano kati ya nchi zilizoendelea ambazo ndiyo wachafuzi wakubwa wa mazingira na nchi zinazoendelea kutoka Afrika.


Rais alizitaka nchi za Afrika zilizoathirika na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza kasi ya kuzibana nchi tajiri ili zikubali kuchangia kwa kiasi kikubwa rasilimali za kubabiliana na athari hizo kwa sababu zinachangia asilimia 97 ya uchafuzi wa mazingira.


“Wao wanachangia asilimia 97 kuchafua mazingira na kusababisha mabadiliko ya tabianchi, sisi tunachangia asilimia tatu. Hivyo, tunawataka wabebe mzigo mkubwa zaidi katika kurekebisha hali hiyo kuliko sisi kwa misingi ile ya wajibu wa pamoja lakini ulio tofauti,” alisema Rais Kikwete.


Aliongeza kuwa wakati wa uongozi wake, Bara la Afrika limeongeza uhusiano na washirika mbalimbali duniani katika kusimamia umuhimu wa kukabiliana kwa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...