MWAKILISHI wa Magomeni visiwani Zanzibar, Salmin Awadhi Salmin (CCM), amefariki dunia ghafla baada ya kuanguka katika kikao cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichokuwa kinafanyika katika ofisi kuu ya chama hicho, Kisiwandui mjini Unguja.
Taarifa hiyo ilianza kuenea mjini Unguja jana saa 6 mchana, na hata kuzua maswali kutoka kwa wananchi kuhusu utata wa kifo chake.
Salmin (57) ambaye pia alikuwa ni mnadhimu wa wawakilishi wa CCM na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho (CC), alikuwa mmoja wa wawakilishi wanaopinga mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa kutaka wananchi waulizwe kama bado wanahitaji muundo huo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu kifo cha mwakilishi huyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vua Ali Vuai, alisema kabla ya kufikwa na mauti, alianguka ghafla wakati akitoka katika kikao hicho cha kawaida.
Alisema baada ya kuanguka viongozi na wanachama walimnyanyua na kumkimbiza Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu.
“Baada ya Salmin kuanguka, baadhi ya viongozi na wafanyakazi kwa haraka walimbeba na kumpeleka katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu na baada ya kufikishwa alipelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), ambako baada ya muda mfupi madaktari walithibitisha kuwa amefariki dunia kwa maradhi ya shinikizo la damu.
“CCM imepokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha kiongozi wetu ambaye alikuwa ni kiongozi na mtendaji wa kuigwa ndani na nje ya chama chetu, ila kazi ya Mungu haina makosa, jambo la kusikitisha amefariki akiwa katika utendaji wa kazi za chama hapa ofisi kuu Kisiwandui,” alisema Vuai.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM alisema kwa sasa taratibu za mazishi zinaandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na chama nyumbani kwake Mpendae na anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja saa 7 mchana.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Wawakilishi (BLW), Yahya Khamis Hamad, alisema baraza hilo limeondokewa na kiongozi mahiri ambaye muda wote alikuwa na kazi ya kuimarisha umoja kwa Wazanzibari.
Salmin Awadh Salmin alizaliwa mwaka 1958 kisiwani Unguja na kusoma Shule ya Msingi Makunduchi kabla ya kuwa kiongoni Wilaya ya Kusini Unguja.
Pia amewahi kushika wadhifa mbalimbali ndani ya CCM ikiwamo ujumbe wa NEC, Kamati Kuu na Mnadhimu wa Wawakilishi wa Kambi ya CCM ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Machi 2, mwaka jana wakati wa mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Salmin aliwaongoza wawakilishi wa CCM kupinga hatua ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, kuwasilisha maoni kwa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya kutaka Serikali tatu na kuyaita ni maoni ya baraza hilo.
Katika mkutano huo, Salmin alisema mapendekezo hayo ni kinyume na msimamo wa CCM na wao hawako tayari kuliona hilo huku akiahidi suala hilo kufikishwa katika vikao vya ngazi za juu.
Salmin alisema Spika Kificho hakuwashirikisha wenzake katika mapendekezo ya Serikali tatu aliyoyawasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakisema Baraza la Wawakilishi, kama taasisi, halikutoa msimamo wa pamoja.
Mei 4, mwaka jana, Salmin alisema wawakilishi wa CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza la Wawakilishi ili kuwapa nafasi wananchi waulizwe iwapo wanataka kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), au la.
Kauli hiyo aliitoa wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho ulioongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana kwenye viwanja vya Kibandamaiti, Unguja.
Salmin alisema wajumbe hao wamefikia hatua hiyo kwa kuwa wanaona kwamba lengo na matumaini ya kuundwa SUK yamefutika na hayana dalili njema katika siku za usoni.
Alisema ni vyema wananchi wakaulizwa kama bado wana hamu na mfumo huo au ule wa zamani urejeshwe.
Katika mkutano huo, alimwomba Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kuunga mkono hoja hiyo itakapowasilishwa ili kutoa nafasi mpya ya kidemokrasia kwa wananchi wake kujua kama wanataka mfumo wa sasa au wa zamani.
0 comments:
Post a Comment