Magu. Matukio ya ujambazi na mauaji ya kutumia silaha, yameanza kuibuka kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hali hiyo imekuwa ikihojiwa na wananchi na wapenda amani na zaidi ni kuhusu intelijensia ya polisi kushindwa kugundua mipango ya uhalifu.
Wachunguzi wa mambo wanasema kuwa kushamiri kwa matukio hayo kunaleta hofu katika jamii huku jamii yenyewe ikilaumiwa kwa kukaa kimya kwa watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na hutumia isivyo halali.
Hali hiyo imetokea mjini Magu, mkoani Mwanza kwa watu wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za moto usiku wa kuamkia jana walifunga Mtaa wa Kisesa Kata ya Kisesa, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza na kumuua mfanyabiashara Nestory Andrew umbali wa mita 50 kilipo Kituo cha Polisi.
Tukio hilo lilitokea saa 8:00 usiku, majambazi hayo yalifunga Barabara ya Mwanza-Musoma kwa muda na kusababisha taharuki kwa wakazi wa Kisesa huku milio ya bunduki ikitawala anga.
Wakizungumza na Mwananchi eneo la tukio jana, mashuhuda walisema walianza kusikia milio mizito ya vitu kama bomu na kwamba baada ya muda wakaona watu wakivamia duka la mfanyabiashara huyo na kupiga risasi hewani.
Mmoja ya mashuhuda hao, Daud Mwalimu alisema “Mimi ni fundi baiskeli hapa stendi jana (juzi) muda kama wa saa mbili usiku nilisikia sauti ya vishindo kama bomu, lakini baada ya muda nikasikia sauti za bunduki hewani,”
Aliongeza: “Kwa kweli tulitawanyika watu wote hapa mtaani na kuacha mali zetu. Baada ya kutulia tulikuja kushuhudia nini kilitokea, lakini tulikuta mtu mmoja ambaye ni mfanyabiashara hapa Kisesa anavuja damu tulimuangalia tukamkuta amefariki.”
Shuhuda mwingine, Emmanuel Juke alisema watu hao walifunga Barabara ya Mwanza-Musoma na kwamba, walikuwa wakipiga risasi ovyo hewani.
Juke alisema hali ilikuwa mbaya, kwani hawakuwahi kushuhudia tukio kama hilo na mtu aliyefariki alikuwa mfanyabiashara maarufu Kisesa.
Mwandishi w habari hizi jana alifika Kituo cha Polisi Kisesa ambako askari wa kituo hicho walikiri kuwapo kwa tukio hilo huku wakitaka atafutwe Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Magu.
Kamanda w Polisi Magu, Charles Mkapa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini akadai msemaji mkuu ni Kamanda wa Polisi Mwanza.
0 comments:
Post a Comment