2015-02-18

Mama aliyeporwa mtoto albino afanyiwa upasuaji wa kichwa



Geita/Dar. Mama wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ambaye alitekwa juzi na watu wasiofahamika mkoani Geita, amefanyiwa upasuaji wa kichwa na jopo la madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) mjini Mwanza.


Mama huyo aliyefahamika kwa jina la Ester Jonas (30), alilazimika kufanyiwa upasuaji huo baada ya kushambuliwa kwa kukatwa mapanga na watu hao ambao walimteka mtoto wake juzi akiwa amembeba mgongoni nyumbani kwake.


Mkuu wa Kitengo cha dharura cha Hospitali ya Bugando, Dk Darick David alisema mama huyo alifikishwa hapo jana akiwa na hali mbaya kutokana na kuvuja damu nyingi.


“Namkumbuka mwanangu Yohana Bahati,” hayo ni maneno aliyoyasema mama mzazi wa mtoto huyo akiwa hospitalini hapa kwenye chumba namba 903 cha uangalizi maalumu (ICU).


“Kama mnavyomuona hali yake siyo nzuri, hata kuzungumza hawezi, alikatwa panga kichwani jeraha kubwa liko puani, tumelazimika kumfanyia upasuaji wa kichwa ili kusafisha damu iliyokuwa imeganda ndani,” alisema Dk David na kuongeza: “Bado anatatizo kubwa na madaktari bingwa wanaendelea kumchunguza.”


Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Profesa Alfred Mteta alisema: “Inasikitisha kuona binadamu unamfanyia unyama binadamu mwenzako, kamwe vitendo hivi haviwezi kukubalika tumempokea mgonjwa huyu na madaktari wanaendelea kumpatia matibabu ili kuokoa maisha yake.”

Mbunge Viti Maalumu


Mbunge wa Viti Maalumu anayewawakilisha watu wenye ulemavu wa ngozi bungeni, Al-Shaymaa Kwegyir ametaka nguvu zinazotumiwa na polisi kuwakamata majambazi, zitumike pia kuwasaka wanaoteka na kuwaua watu wenye ulemavu huo.


Kauli ya Kwegyir imekuja baada ya kuanza kuibuka kwa matukio ya utekaji na kuwaua wenye ulemavu wa ngozi kwa imani za kishirikina.


Hivi karibuni, mtoto mwingine mwenye ulemavu wa ngozi mkoani Geita alitekwa na mama yake kucharangwa mapanga. Utekaji huo umetokea ikiwa ni siku 50 sasa tangu kutoroshwa kwa mtoto, Yohana mkoani Mwanza.


“Polisi wana nguvu za kukamata majambazi, kwanini nguvu hiyo isitumike kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivi, tumeanza kuwa na shaka juu ya utendaji kazi wao kuwa unaegemea upande fulani,” alisema Kwegyir.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...