2015-02-18

Makaidi kuwania urais kupitia Ukawa...........ni hatariiiiiiiiiiiiiiiiiiii


Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi.

Asema wanachama wake wamridhia na kupendekeza jina lake kuwa miongoni mwa watakaoshindanishwa katika umoja huo

Dar es Salaam. Wakati vyama vingine vinavyounda Ukawa, vikiendelea na mchakato wa kutafuta jina litakalopendekezwa kuchukua kiti cha urais, Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi amesema, tayari chama chake kimeshapendekeza jina lake kuwa miongoni mwa vigogo watakaoshindanishwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Ili kupatikana jina la mgombea mmoja atakayechukua nafasi hiyo, makubaliano ya umoja huo yanaelekeza vyama kupendekeza jina moja litakalowakilishwa katika Kamati ya Wataalamu ya Ukawa kabla ya kushindanishwa na majina mengine.

Katika harakati za kutafuta jina la mgombea mmoja, wenyeviti wenza wa Ukawa walikuwa wakifanya mikutano mara kadhaa na Januari mwaka huu walifikia makubaliano ya kuanza mapema kwa mchakato huo.

Mkutano huo ulielezwa kuwa na ajenda kadhaa ikiwamo changamoto ya uandikishaji wa Daftari la Wapigakura, hali ya uchumi na suala la mgombea urais kupitia umoja huo. 

Hata hivyo, Vyama vya NCCR Mageuzi, CUF na Chadema bado havijaonyesha mwelekeo wa kupatikana jina la mgombea wa urais kutokana na michakato inayoendelea ndani ya vyama hivyo.

Jana, Dk Makaidi alisema kwamba wanachama wa chama hicho wameridhishwa na uwezo, ushawishi wake hivyo kupendekeza jina lake kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais kupitia Ukawa.

“Kwa hivyo baada ya kuungana na Ukawa, wanachama wakabariki jina langu lipelekwe kwenye umoja huo,” alisema na kuongeza;

“Mkutano uliopita tulikubaliana kwamba, jina la mgombea mmoja wa urais kupitia Ukawa lazima lipatikane mwishoni mwa Aprili…Makubaliano hayo yalitokana na mkutano wa wenyeviti wa Januari mwaka huu.”

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya alisema katika mkutano huo walikubaliana mpaka kufikia Mei, vyama vyote viwe vimekamilisha taratibu zote ili kuanza mchakato wa kutafuta jina la mgombea urais wa Ukawa. 

Katika hatua nyingine, Sakaya alikanusha taarifa zilizoripotiwa hivi karibuni kwamba, jina la Profesa Ibrahim Lipumba limepitishwa na chama hicho.

“Utaratibu utakaoanza kwa sasa ni uchukuaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za urais, ubunge na udiwani kupitia kura ya maoni ndani ya chama,” alisema na kuongeza:

“Jina la mgombea urais haliwezi kupitishwa na kutangazwa bila kufuata kanuni…Lazima lijadiliwe kwenye vikao kuanzia vya wakurugenzi wa chama mpaka Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la chama na hatua hiyo inaweza kufanyika Mei au Aprili mwishoni.”
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...