2015-02-18

Waogombea urais kupitia Ukawa wajitokeze tuwaone


 
Kwa nini mpaka sasa wanachama wa umoja huo hawataki kujitokeza hadharani kutangaza nia kama ilivyo kwa wenzao wa CCM?

Je, ni kutekeleza msemo wa kimya kingi kina mshindo? Kwamba Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unasubiri kuja kuwashangaza Watanzania.

Kwa nini mpaka sasa wanachama wa umoja huo hawataki kujitokeza hadharani kutangaza nia kama ilivyo kwa wenzao wa CCM?

Tayari makada maarufu wanne wa CCM wameshatangaza rasmi nia ya kuomba ridhaa ya chama chao kugombea, huku wengine zaidi ya 10 licha ya kutotangaza, harakati zao zinadhihirisha bayana kuwa wana dhamira ya kugombea kiti hicho.

Pamoja na kupanda kwa joto la Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba, makada wa vyama vinavyounda Ukawa wamekaa kimya, suala linaloonekana kutowaridhisha baadhi ya watu.

Baadhi ya watu hao wakiwamo wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema vyama vinavyounda Ukawa na kambi ya upinzani kwa jumla havina budi kuvunja ukimya na kuwaweka hadharani ‘watarajiwa’ wao.

Padri Baptist Mapunda ni miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya siasa nchini ambaye anasema wakati umefika kwa wapinzani nao kuweka hadharani wagombea wake ili kutoa fursa kwa wananchi kuwajua na kuwapima.

“Sioni sababu ya wanaouunga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) au kambi ya upinzani kwa jumla kuwa kimya kuhusu kutoa ruhusa au hata kuwahimiza wafuasi wake wenye nia ya kugombea nafasi ya urais kuanza mapema,’’ anasema na kuongeza”

“Wajitokeze wenye nia kutoka Chadema, CUF au NCCR-Mageuzi au NLD…Kila mmoja aeleze sababu za kujitosa, kwa nini anajiona anafaa na anaweza, anakusudia kuleta mabadilikko yapi, nini malengo yake…Hii itatoa fursa kwa wananchi kupate muda wa kuwajua na kuwapima.

Anasema anayetafutwa ni Rais wa nchi hivyo Watanzania wanayo haki ya kumjua mapema na kumpima kama anayo sifa au hana na kuongeza kuwa vyama vinaweza visijue udhaifu wa wanachama na viongozi wao, lakini wananchi wana uwezo wa kubaini upungufu wa wagombea.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi, tangu Januari wenye nia ya kuomba nafasi zozote za uongozi walipaswa kueleza nia zao hadharani ili kutoa fursa kwa wananchi kuwajua na kuwapima Watanzania wenzao wanaotaka kuwaongoza” anaeleza Mapunda.

Anasema ile dhana kuwa wapinzani ni watu safi na wasio na doa haina mashiko katika suala hili, kwa kuwa hakuna binadamu aliyekamilika.

“Anaweza kuwa mgombea mzuri asiye na doa kutoka upinzani, lakini akawa hana vision (maono) wala mkakati wowote wa kuinua uchumi wa wananchi. Mtu wa namna hiyo hawezi kutufaa na usafi wake maana anayetakiwa ni kiongozi mwenye mtazamo wa kuiendeleza Tanzania yetu na watu wake,” anafafanua.

Katibu mkuu wa zamani wa NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza anasema ukimya huo wa kambi ya upinzani ni udhaifu mkubwa unaoweza kusababisha upinzani uonekane kukosa mwelekeo.

Anaeleza kuwa imekuwa kawaida kwa wapinzani kusubiri CCM waweke mgombea wao hadharani ndipo wao waje nyuma na kuanza kutangaza, jambo analosema linawanyima wafuasi fursa ya kuwapima wanachama watakaogombea kutoka kambi hiyo.

“Kwa hali hii, naona bado wapinzani nchini hawajawa na mwelekeo. Kwa sasa ambapo kuna muungano wa Ukawa, naweza kusema labda hawajajua hatima ya ukawa maana wapinzani kwa kawaida hawajazoea upinzani kushirikiana katika uchaguzi,” anasema. 

Anaongeza kuwa ipo dhana iliyojengeka kwa wafuasi wa upinzani kuwa wagombea wake wanajulikana na hivyo kuwapa hofu wafuasi wengine kujitokeza na kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo ya ya juu uongozi wa nchi.

“Wakati mwingine ni hofu kuwa, nikijitokeza nitashindana na Dk Willibrod Slaa au Profesa Ibrahimu Lipumba. lakini kumbe hata wao inawezekana hawajatangaza. Binafsi sioni haja ya woga huu. Ni kwamba watu hawajajiamini na wanaviziana, nani aanze” anasema na kuongeza:

“Mtu yeyote anayejiona anafaa kutangaza aseme, kama mimi ni NCCR nikitangaza kugombea siwezi kuingiliwa na CUF wala Chadema. Mwishowe wagombea wote watapambanishwa na Ukawa kuamua nani watakayemsimamisha.”

Je, kutangaza mapema kuna faida?
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...