2015-02-09

Mwanafunzi Aliyebakwa na Polisi Adaiwa Kutoroshwa ili Kuficha Ushahidi



 
MWANAFUNZI wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 15 anayedaiwa kubakwa na askari wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, usiku wa kuamkia Januari 6 mwaka huu, ametoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Tukio la kubakwa mwanafunzi huyo (jina tunalo), aliyekuwa aingie kidato cha pili Sekondari ya Sakwe, iliyopo Bariadi, mkoani Simiyu, lilitokea eneo la Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga.

Walezi wa mwanafunzi huyo, wamedai kuwa kitendo cha kutoweka binti yao kimelenga kuharibu ushahidi wa kesi ya ubakaji uliofanywa na askari wa jeshi hilo. 

Mama mdogo wa mwanafunzi huyo, Neema Elisha, alisema mtoto huyo alitoweka nyumbani kwake na baada ya kumtafuta walimkuta mikononi mwa polisi hali ambayo iliwashangaza na kuwapa hofu kwa kuwa askari polisi ndiye mlalamikiwa.

"Januari 10 mwaka huu, aliondoka nyumbani bila kuaga, tulimtafuta na baada ya kutoa taarifa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) ilibainika yupo Kituo cha Polisi Mjini Shinyanga akidai aliondoka nyumbani kwa sababu tulikuwa tunampiga madai ambayo si ya kweli.

"Baadaye kulifanyika kikao lakini sisi tulitolewa nje akabaki mtoto, watu wa Shirika la Agape na polisi tukaelezwa mtoto hatorudi tena nyumbani na kuanzia siku hiyo, atatunzwa na Ofisi ya Ustawi wa Jamii," alisema Elisha.

Aliongeza kuwa, alipoulizwa sababu za kutorudi nyumbani wakaambiwa mtoto mwenyewe ndiye amekataa kurudi nyumbani kwa hofu ya kupigwa.

"Tangu Januari 10, mwaka huu hadi sasa, hatufahamu mtoto yuko wapi, tunapokwenda polisi kuulizia tunafukuzwa na kuambiwa mtoto huyo amepelekwa Bariadi kwa bibi yake na ameanza masomo maelezo ambayo si ya kweli kwani tumewasiliana na watu wa Bariadi wamesema hayupo na shuleni anatafutwa," alisema. 


Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia mkoani humo, Pili Misungwi, alisema mwanafunzi huyo yupo katika mikono salama wilayani Bariadi ambako alisafirishwa na basi la Kampuni ya Mombasa Raha kwa kumkabidhi kondakta wake anayeitwa Yohana.

Kondakta huyo alikiri kupewa mwanafunzi na askari ambaye alimtaja kwa jina moja la Ruthi aliyeambatana na Ofisa Ustawi wa Jamii ambaye hakufahamika jina ili amsafirishe kwa kuhakikisha anamteremsha Kituo cha Mabasi Bariadi.

"Ni kweli walinikabidhi huyo mtoto, nilichoelezwa nihakikishe namfikisha Bariadi, nichunge asiteremke njiani na ndicho nilichofanya, tulipofika kituo cha mwisho wa lami Mjini Bariadi aliteremka na mwenyewe alidai anafahamu anakokwenda, sisi tulimuacha hapo maana sikuelekezwa nimkabidhi kwa mtu," alisema Yohana.

Waandishi wa habari walibahatika kuwasiliana na bibi wa mtoto huyo anayeishi Bariadi kupitia simu yake ya kiganjani ambaye alijitambulisha kwa jina la Mama Neema na kusema mjukuu wake hajafika nyumbani, hafahamu anakoishi kwa sasa na shuleni kwao bado wanamtafuta.

Pia mwanafunzi huyo alipatikana katika namba ya simu iliyotolewa na Ruth wa Dawati la Jinsia mkoani humo na kudai yupo Bariadi na ameanza masomo japo hakuweza kueleza ni lini atarudi Shinyanga kufuatilia kesi yake mahakamani akidai hajaelezwa tarehe ya kesi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Longinus Tibishubwamu mbali ya kusikitishwa na taarifa za kutofahamika aliko mwanafunzi huyo, aliahidi kulifuatilia suala hilo kwa kufanya uchunguzi wa kina na ndani ya siku mbili atahakikisha anapatikana na kukabidhiwa mikononi mwa wazazi wake.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...