Mwanaume mmoja Yusufu Chatambala (45) mkazi wa Kijiji cha Makutupa Kata ya Lupeta Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukiri kosa la kumbaka mtoto mdogo mwenye umri wa miaka minne.
Mwendesha mashtaka wa polisi Godwill Ikema ameiambia mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Feb 20 mwaka huu majira ya saa 12 jioni katika kijiji cha Makutupa kilichopo Wilayani Mpwapwa ambapo alimbaka mtoto mdogo wa kike mwenye umri wa miaka minne (jina limehifadhiwa).
Mwendesha mashtaka huyo amesema kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha sheria za nchi chini ya Kifungu namba 130 (1) 2 (a) na 131 (1) cha Kanuni ya Adhabu kama kilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002.
Amesema kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo baada ya kumkamata alipokuwa akicheza na watoto wenzake jirani na nyumbani kwao kisha kumpeleka kwenye shamba la mahindi kisha kumbaka mtoto huyo na kusababishia majeraha na maumivu makali.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa Paschal Mayumba alimtia hatiani mtuhumiwa huyo jana baada ya kukiri kutenda kosa hilo.
Akisoma hukumu hiyo, hakimu Mayumba amesema Mahakama inamhukumu kwenda jela kifungo cha maisha kwa kosa la kubaka mtoto ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wanaotenda makosa kama hayo.
0 comments:
Post a Comment