Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete akipiga makofi wakati alipowasili katika mkutano wa chama hicho Mjini Dodoma hivi karibuni.
Adhabu ya makada sita wa CCM ya kufungiwa miezi 12 ilishaisha tangu kastikati ya mwezi huu na sasa wanasubiri kwa hamu tangazo la Kamati Kuu la kumalizika kwa adhabu yao ili wawe huru kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho na kuendelea na shughuli nyingine za kujiandalia mazingira ya kupitishwa na Halmashauri Kuu.
Dar es Salaam. Wakati makada wa CCM wakivuta pumzi ya mwisho kwa matarajio ya kuondolewa kifungo cha miezi 12 ili wajitose rasmi kuwania urais, Kamati Kuu ya chama hicho inakutana leo kukiwa na habari kuwa itatumia muda mwingi kujadili mwelekeo wa mchakato wa Kura ya Maoni na badala wa wanachama hao sita.
Adhabu ya makada sita wa CCM ya kufungiwa miezi 12 ilishaisha tangu kastikati ya mwezi huu na sasa wanasubiri kwa hamu tangazo la Kamati Kuu la kumalizika kwa adhabu yao ili wawe huru kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho na kuendelea na shughuli nyingine za kujiandalia mazingira ya kupitishwa na Halmashauri Kuu.
Makada hao ni Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, ambao waliwahi kuwa mawaziri wakuu, William Ngeleja, Steven Wasira, ambaye ni Waziri wa Kilimo na Chakula, na January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia.
Hadi sasa makada hao, ambao walituhumiwa kuanza harakati za kampeni kabla ya muda, hawajatangaza rasmi nia ya kuwania urais na habari zinasema kuwa wamekuwa kwenye maandalizi ya kufanya hafla kubwa ya kutangaza mpango huo.
Lakini habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema kuwa kuna uwezekano mdogo wa Kamati Kuu kuzungumzia suala hilo kwa kuwa kikao hicho kitajikita zaidi kuzungumzia mwenendo wa mchakato wa Kura ya Maoni ambao unaonekana kuyumba.
“Watu wameandika sana kuhusu Kamati kufanya uamuzi wa wagombea urais waliofungiwa, lakini nakuhakikishia suala hilo halitazungumzwa labda iweje sijui,” alisema mpashaji habari wetu aliye ndani ya chama hicho.
“Suala linalosumbua kwa sasa ni Kura ya Maoni na hilo ndilo litachukua muda mwingi.”
Alisema kamati Kuu itatoa mwelekeo wa Kura ya Maoni, ambayo mchakato wake unapingwa vikali na vyama vya upinzani ambavyo vinasema uchache wa vifaa, muda mdogo wa maandalizi, watendaji na matumizi ya teknolojia ya uchukuaji wa taarifa za wapigakura kuwa vinaweza kfanya kazi ya uandikishaji kuchukua muda mrefu na hivyo Kura ya Maoni isipigwe Aprili 30 kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete.
Kada mwingine wa chama hicho pia aliidokeza Mwananchi kuwa wagombea hao waliofungiwa watabidi kuvuta pumzi zaidi kabla ya kuachiwa huru rasmi.
Mmoja wa wasaidizi wa kada aliyefungiwa alipoulizwa kuhusu mipango ya bosi wake kutangaza rasmi kugombea, alisema: “Sisi tunaisubiri Kamati Kuu tu. Ikitangaza kumalizika kwa adhabu tu, hata wiki ijayo tutatangaza rasmi.”
Alipoulizwa kuhusu kikao hicho cha leo, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye hakutaka kuzungumzia ajenda.
Hivi karibuni, Nape alithibitisha kuwa muda wa adhabu hiyo ulikuwa ukingoni na kuwa viongozi hao sita wangefanyiwa tathmini na kamati ndogo ya maadili ili kubaini iwapo adhabu hiyo ilitekelezwa ipasavyo.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment