Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma leo linaanza kumhoji mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kutokana na kutajwa kwenye sakata la uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, akiwa mmoja wa watu kadhaa watakaofika kwenye Ukumbi wa Karimjee kwa mashtaka tofauti.
Si mzungumzaji sana kwenye vikao vya Bunge na hivyo haandikwi sana na vyombo vya habari, lakini kunapotokea masuala mazito, jina lake hung’ara na wengi kujiuliza Chenge ni nani anayeweza kupita kirahisi kwenye masuala kama hayo.
Mbali na sakata hilo la escrow, Chenge alitajwa pia katika kashfa ya ununuzi wa rada, ambayo ilimlazimu kuachia uwaziri.
Akiwa ni msomi aliyehitimu Shahada ya Umahiri wa Sheria kwenye Chuo Kikuu cha Harvard cha Marekani -- moja ya vyuo bora kabisa duniani-- Chenge amekuwa nadhifu katika mambo yake na ni mara chache sana waheshimiwa wabunge hujitokeza na kumtuhumu waziwazi kuhusika kwenye kashfa.
Wakati akichangia moja ya mijadala kwenye Mkutano wa 16/17 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Halima Mdee alijaribu kumtaja Chenge waziwazi kuwa anahusika katika kila mikataba yenye matatizo, lakini mwanasheria huyo wa zamani alimzima kwa kuomba mwongozo na kumtaka spika amlazimishe mbunge huyo wa Kawe awasilishe ushahidi wa anachokisema, la sivyo aache kuchafua watu.
Mdee hakuweza kuwasilisha na badala yake, akaachana na hoja hiyo na kuendelea na mambo mengine. Siku hiyo, mwanasheria huyo alionekana kuchukizwa na kwa mwonekano wa sura yake alipania kutumia umahiri wake wa kisheria kukomesha shutuma zinazorushwa kwake mara kwa mara, lakini kitendo cha Mdee kutoendelea kilimrudisha nyuma. Lakini hiyo haikuondoa ukweli kuwa Chenge alitajwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada ambayo ilichunguzwa na kitengo cha makosa makubwa ya jinai cha Uingereza kilichokuwa kikichunguza uamuzi wa Tanzania kununua kifaa hicho cha mawasiliano kwa bei kubwa wakati Serikali ikishindwa kutoa huduma kwa wananchi.
Rada hiyo ilinunuliwa kutoka kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa Dola 40 milioni mwaka 2001, kiwango kilicholistua hadi Bunge la Uingereza.
Katika uchunguzi wa suala hilo, ilibainika kuwa Chenge alikuwa na akaunti kwenye kisiwa cha Jersey iliyokuwa na zaidi ya Dola 1 milioni (sawa na zaidi ya Sh1.8 bilioni kwa kiwango cha sasa).
Kinachofanya Chenge awe gumzo, ni jinsi alivyopita kirahisi kwenye kikwazo hicho. Alijiuzulu wadhifa wake wa Waziri wa Miundombinu.
Wakati kashfa hiyo imepamba moto mwaka 2008, Chenge alikuwa ziarani China akiwa na Rais Jakaya Kikwete na aliporejea aliwaambia waandishi waliomzonga kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwa fedha hizo ni “vijisenti”. Baadaye aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kujitetea kuwa ni muadilifu, mtu safi na hakutenda kosa katika kashfa hiyo.
Katikati ya kashfa hiyo, Chenge alihusika katika ajali iliyoua watu wawili, mmojawapo akisemekana kuwa ni mtu waliyekuwa wakifahamiana sana. Alishtakiwa kwa makosa ya kuendesha kizembe na kuendesha gari bila ya kuwa na bima. Alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh700,000 ambazo alilipa.
Miaka nane baadaye, Chenge alijikuta kwenye sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow. Zaidi ya Sh306 bilioni zilichotwa na mikono ya Chenge haikuonekana hadi ulipofuatiliwa mgawo wa fedha hizo zilizotoka Benki Kuu. Ilibainika kuwa aliingiziwa Sh1.6 bilioni na aliyekuwa mmoja wa wamiliki wa IPTL, kampuni ambayo iko katikati ya kashfa hiyo.
0 comments:
Post a Comment