Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
Amesema sheria ya maadili ya viongozi wa umma haina nguvu ya kukabiliana na mmomonyoko huo na inakosa meno kwa sababu inasimamiwa na watu walewale wasiotaka ‘kuguswa’.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema nchi haiwezi kupambana na mmomonyoko wa maadili ya viongozi wa umma kama haitakubali kuingiza suala la maadili katika Katiba.
Amesema sheria ya maadili ya viongozi wa umma haina nguvu ya kukabiliana na mmomonyoko huo na inakosa meno kwa sababu inasimamiwa na watu walewale wasiotaka ‘kuguswa’.
“Kuna mambo yanakataliwa sasa hivi, lakini kuna siku lazima yatakuja kuingizwa katika Katiba, mfano ni suala la maadili,” alisema Jaji Warioba wakati akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na ITV juzi usiku.
“Hatuwezi kuendelea kama ilivyo sasa bila kuchukua hatua kali na nzito kushughulikia maadili. Lazima kuna siku suala hili litaingia katika Katiba tu,” alisema.
Jaji Warioba ametoa kauli hiyo ikiwa zimepita siku mbili tangu Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutaja viongozi wa umma itakaowahoji kutokana na kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Miongoni mwao yupo kigogo wa Ikulu mwenye cheo cha mnikulu, Shaban Gurumo, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na mwanasheria mkuu wa zamani, Andrew Chenge.
Katika rasimu ya pili ya Katiba, Tume ya Jaji Warioba ilipendekeza miiko na kanuni za uongozi kama tunu za Taifa, lakini Bunge Maalumu la Katiba iliyaondoa na kuyaweka katika msingi wa utawala bora.
Mara kadhaa Jaji Warioba amekuwa akihoji kuwa uzalendo na uadilifu si mpaka mtu awe kiongozi, kwamba mambo hayo mawili si misingi ya utawala bora ni misingi ya kitaifa na inamhusu kila Mtanzania.
Akifafanua zaidi suala la maadili katika kipindi hicho, Jaji Warioba alisema tume yake iliangalia sheria ya maadili ikaona haina nguvu sana na inategemea kiongozi mmoja na ndiyo maana waliingiza suala hilo katika rasimu ya Katiba
“Tuna sheria ya maadili lakini haina nguvu kwa sababu wanaoisimamia ni walewale. Nchi za Ufilipino (Philippines), Afrika Kusini, Namibia na Kenya walikuwa na sheria lakini haikuwa na nguvu na iliwahusu watu walewale. Waliamua kuweka maadili katika Katiba ili waweze kulitekeleza vizuri,” alisema.
Alisema maadili pia yanawahusu viongozi lakini wakati huo huo viongozi hao ndiyo wanaosimamia sheria ya maadili, hivyo hawawezi kukubali liwemo jambo litakalowadhuru.
Jaji Warioba alieleza jinsi Azimio la Arusha lilivyokuwa na nguvu, akifafanua kuwa suala la maadili lilijipambanua wazi na waliokuwa wakitenda mambo kinyume walijiondoa wenyewe bila kusubiri kuondolewa.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment