Stori: Saimeni Mgalula, MBEYA
DUNIA ina mambo jamani! Mtoto Cecilia Yessa, 6, (pichani) ni bubu na kiziwi tangu kuzaliwa, lakini baba yake mzazi, Yessa Vincent (39), mkazi wa Kijiji cha Igawa, Kata ya Lugelele wilayani Mbarali mkoani hapa amesimulia maajabu yaliyotokea mpaka mtoto wake kupata ulemavu huo.
Akizungumza na paparazi wetu hivi karibuni nyumbani kwake, baba huyo alisema wakati mkewe aliyemtaja kwa jina moja la Hafsa akiwa mjamzito, alikumbwa na mapepo yaliyosababisha kumpiga mwereka mara kwa mara.
AENDA KWA MGANGA WA KIENYEJI
Akiendelea kuelezea mkasa huo, baba huyo alisema: “Baada ya kuona hali hiyo ikiendelea kumtokea kwa kasi mke wangu niliamua kwenda kwa mganga wa kienyeji kuagua ili tujue tatizo ni nini.
“Nilikwenda kwa mganga huyo katika Kijiji cha Muungano ambacho kipo wilaya hiihii. Mganga aliniambia kuwa, mapepo aliyonayo mke wangu ni ya mtu ambaye alikuwa ana matatizo ya mikosi ambaye naye alitupiwa dawa akaogee katikati ya njia panda saa nane usiku huku akiwa ameangalia upande wa mashariki.
“Mganga aliendelea kuniambia kuwa, mtu huyo aliambiwa dawa hiyo aogee akiwa mtupu, yaani kama alivyozaliwa huku akisema, ‘nimechoka na kukaa na mzigo huu naomba nipokelewe na binadamu yeyote au mnyama,’’ alisema baba huyo akimkariri mganga wake.
MKE APITA, ABEBA UCHAWI
Kwa mujibu wa baba huyo, mganga alimwambia huenda mkewe alipita njia hiyo baada ya mtu huyo kuoga ndipo akapokea mzigo huo.
“Nilipewa dawa za kumnywesha mke wangu ili kumuepusha na tatizo hilo. Dawa zile zilimsaidia akaacha kupiga mwereka mara kwa mara na kuonekana ameanza kupona,” alisema.
MKE AJIFUNGUA, MATATIZO TENA
Yessa aliendelea kusema kuwa, baada ya miezi tisa mkewe alijifungua mtoto huyo wa kike. Alizaliwa akiwa vizuri lakini baada ya miezi mitatu mtoto na mama yake walianza kusumbuliwa tena na matatizo ya mapepo, mama alikuwa akipiga mwereka kila mara, mtoto naye vivyo hivyo.
“Safari hii niliamua kuzunguka nao sehemu mbalimbali za waganga wa tiba asilia ili kuwaepusha na janga hilo, bahati mzuri mganga mmoja alisaidia hali ikatulia.
CHA AJABU SASA
“Lakini cha ajabu, baadaye tena tatizo lile likaendelea kumrudia mke wangu. Mwereka kila wakati. Mbaya zaidi, mtoto wangu naye akaanza dalili za kutosikia na kushindwa kusema chochote, yaani ni bubu na kiziwi kwampigo.
“Nachotaka kusema mpaka nikaamua kutafuta chombo cha habari, hawa waganga wanautesa sana ulimwengu. Kama kweli mtu anapona, kuondolewa mikosi kwa kigezo cha watu wengine wabebe mzogo huo ni shida.
“Ni afadhali basi huo mzigo angebeba mnyama yoyote, hata ng’ombe. Mwanangu huu ni mwaka wa sita sasa, ni bubu na kiziwi,” alimaliza kusema baba huyo.
0 comments:
Post a Comment